Παρασκευή 30 Οκτωβρίου 2015

AFRIKA MAGHARIBI: Hatua za Pamoja Dhidi ya Uharamia



Noël Kokou Tadégnon  

Tayari kuna zaidi ya mashambulizi matatu ya meli yaliyofanywa na maharamia katika Pwani ya Afrika Magharibi mwaka huu. Serikali za kikanda zitakutana mjini Cotonou, Benin mwezi Oktoba kujadili jitihada za pamoja za kutokomeza uharamia.

LOME, Oct 10 (IPS) -
Takwimu za mashambulizi zinatokana na matukio yaliyoripotiwa na waongoza meli kwa Kituo cha Kimataifa cha Kutoa Taarifa za Uharamia Baharini na zinaonyesha tishio linalozidi kuongezeka la usafiri wa meli katika ukanda wenye utajiri wa mafuta.

Mashambulizi ya karibuni zaidi ni yale ya Sep. 15 dhidi ya meli ya mafuta ya Mattheos I ikiwa na wafanyakazi wake 23 katika pwani ya Togo. Siku kumi baadaye, wamiliki wa meli kutoka Hispania waliviambia vyombo vya habari kuwa meli hiyo na wafanyakazi wake wameshaachiliwa huru; bila kulipwa kwa fedha zozote zile zilizodaiwa na watekaji lakini baadhi ya mafuta ya dizeli yaliibwa katika meli hiyo.

Serikali katika mwambao wa Afrika Magharibi zimeonyesha wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa idadi ya mashambulizi dhidi ya meli za mizigo, na zinataka kukusanya rasilimali chache walizonazo kuendesha hatua za pamoja, kama vile kushika doria katika Ghuba ya Guinea.

"Lakini hatutaki kuishia tu kwenye doria za pamoja kati ya Benin na Nigeria; hivi karibuni tutaenea na kuhusisha majeshi ya Togo na Ghana," Kamanda Maxime Ahoyo, mkuu wa Jeshi la Majini la Benin, aliiambia IPS.

"Kama tutakabiliana na matatizo ya uharamia katika maji ya Benin lakini, kwa mfano, tutaacha kuchukua tahadhari za kiusalama katika maji ya Togo, na kama hatutaungana na wenzetu wa Togo na nchi nyingine, hali hii – ambayo ina mtandao mpana – itazidi kuenea."

Madhara ya kiuchumi

Rais wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, James Victor Gbeho, ametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya uharamia na kupanuliwa na kuingiza mataifa yote katika pwani.

"Majeshi ya majini katika mataifa yetu yote ya ukanda wa pwani yanapaswa kuunganisha nguvu zao siku zote," Gbeho aliiambia IPS, huku akisitiza imani yake kuwa tatizo la uharamia lazima kupatiwa ufumbuzi kamilifu. "Hali hiyo inazidi kutisha na inaweza kuwa na madhara makubwa ya kiuchumi kwa nchi zetu. Hii ndiyo sababu tutachukua hatua dhidi yake."

Uharamia tayari umeshasababisha makampuni ya bima ya vyombo vya baharini mjini London kuiingiza Benin katika orodha ya kuwepo katika ukanda wa hatari kubwa ya usafiri wa meli. Makampuni ya bima ya vyombo vya baharini yanayowakilishwa na chama cha ‘Lloyd's Market Association’ yanadai ada kubwa kulipia meli zinazopita katika ukanda huo.

Kulingana na Bénetti Gagalo, Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Walaji cha Togo, hali hiyo ni wazi itakuwa na madhara katika kipato cha bandari za ukanda huo ikiwa ni pamoja na gharama za bidhaa za walaji.

Msaada kutoka nje

Dharula ya hali hiyo imesababisha serikali za kikanda kuomba msaada kutoka Ufaransa na Marekani, ambao wameshapeleka vifaa vya majini katika eneo hilo.

Manuwari ya Kifaransa ya Germinal, tayari inafanya doria katika pwani ya Benin, Togo na Ghana kujaribu na kupunguza uharamia, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa askari wa majini kutoka nchi zote tatu.

"Tumewapatia mafunzo askari hawa wa majini, na wameshiriki katika mazoezi yote ya kiusalama na kufanya doria ambayo tumeyafanya kuzuia uharamia. Na wametusaidia na maarifa yao waliyonayo katika eneo hili la oparesheni," Sébastien Chatelin, nahodha wa manuwari hiyo ya Kifaransa, aliiambia IPS.

Manuwari ya Kimarekani, HSV Swift, pia imefika katika Ghuba ya Guinea, ikisaidia kupambana na uharamaia huku ikitoa mafunzo kwa askari wa majini wa Benin, Togo na Ghana kama sehemu ya mpango wa kijeshi wa Marekani ujulikanao kama "Africa Partnership Station".

"Lengo letu ni kujaribu na kutoa mafunzo kwa washirika wa Afrika juu ya usalama," alisema nahodha wa chombo hicho cha Marekani, Rhett S. Mann.

"Mpango wa APS utaturuhusu kufanya kazi pamoja kukabiliana na matatizo ambayo yanaathiri maji ya pwani yetu," aliongeza Sam Nkruma, ofisa kutoka jeshi la majini la Ghana.

Askari mwenzake wa Benin, Christian Oussa, alikaribisha mafunzo waliyopata wakiwa katika meli mbili za jeshi la majini. "Hii itaturuhusu kukabiliana na uharamia na wafanyabiashara haramu katika bahari. Tumejifunza jinsi ya kupanda meli zinazotiliwa mashaka na kuzikagua; mafunzo ni mazuri mno," aliiambia IPS. (END/2011)


‘Nchi za Afrika ziungane kudhibiti uharamia’

Ili kukabiliana na vitendo vya uharamia kwenye wa Bahari ya Hindi, nchi za Afrika zimetakiwa

Mwananchi


Dar es Salaam. Ili kukabiliana na vitendo vya uharamia kwenye wa Bahari ya Hindi, nchi za Afrika zimetakiwa kuweka nguvu katika ushirikiano, kwa kuwa si rahisi nchi moja kudhitibi uhalifu huo unaofanya na watu wanaodaiwa kuwa ni raia wa Somalia.
Hayo yalisemwa jana na mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga wakati akifungua mkutano wa waendesha mashtaka na wapelelezi wa kesi za uharamia kwa nchi zilizopo ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema kuna baadhi ya meli zinakwepa kupita pwani ya Somalia kwa hofu ya maharamia na kulazimika kuzunguka umbali mrefu.
“Matokeo yake, bei za bidhaa zinazoingizwa na meli hizo zinakuwa juu kutokana na kufidia gharama za usafirishaji zinazotokana na meli kutumia njia ndefu,” alisema Mganga.

DPP alisema meli zinazopita pwani ya Somalia zimekuwa zikitozwa kiasi kikubwa cha bima na kwamba gharama hizo zimekuwa zikifidiwa na watumiaji wa bidhaa zinazoletwa na meli hizo.
“Wakati maharamia wanaungana kufanya uhalifu, nasi kama mataifa tunaoathirika na matukio haya tunatakiwa kuungana ili kupambana nao,” alisema.
Aliwataka waendesha mashtaka na wapelelezi wa masuala ya uharamia kubadilishana uzoefu na mbinu za kushughulikia wahalifu hao ili waweze kuadhibiwa.

Naye, balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Filiberto Sebregondi alisema umoja huo umekuwa ukitoa rasilimali fedha kwa ajili ya kupambana na uharamia kwenye Bahari ya Hindi.
“Tunataka waendesha mashtaka wa makosa ya uharamia katika nchi zilizoko katika pwani ya Bahari ya Hindi, kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuwadhibiti maharamia hawa,” alisema.
Sebregondi alisema maharamia hawana mipaka na kwamba nchi mbalimbali zinatakiwa kuweka mtandao wa ushirikiano ili kuwakamata.
“Ni jambo muhimu kwa nchi husika kuliangalia kwa ukubwa zaidi suala hili, kwa kuwa kinyume chake ni kuruhusu uharamia kuendelea,” alisema.
Mkutano huo unashirikisha waendesha mashtaka kutoka nchi za Tanzania, Somalia, Djibouti Shelisheli, Mauritius, Yemen na Kenya.

Ona pia

Uharamia Afrika Magharibi

Uharamia biashara katika Pembe ya Afrika (2008)

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου