Δευτέρα 12 Οκτωβρίου 2015

Wasomi kizimbani kwa kuchochea njaa nchini


 
Picha hapa

Raia Tanzania

INADAIWA kwamba, Afrika ndilo bara pekee duniani ambalo utabiri wa mwanauchumi mashuhuri Malthus (1798) kwamba uzalishaji wa chakula hautaweza kuwiana na ongezeko la watu umetimia tangu miongo michache iliyopita.

Msingi wa dhana ya Malthus ni kwamba, wakati idadi ya watu inaongezeka kwa kasi ya kutisha, upatikanaji wa chakula unakua kwa kusuasua.
Kilimo huchangia takriban asilimia 50 ya Pato Ghafi la Taifa (GNP) Barani Afrika na kwa Tanzania, mchango wake ni zaidi kidogo ya
asilimia 60, ambapo wakati huo huo takriban asilimia 84 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo.
Takriban asilimia 50 ya Watanzania ni masikini wanaoishi chini ya mstariwa ufukara (poverty datum line) ambapo asilimia 80 yao wanaishi vijijini wakitegemea kilimo kwa maisha yao. Wakati idadi ya Watanzania inaongezeka kwa karibu asilimia 5.2 kwa mwaka, uzalishaji wa chakula unaongezeka kwa asilimia 2.6 tu kwa mwaka. Hapa ndipo utabiri wa Malthus unapotimia.
Katika mada hii, tutazungumzia mgogoro wa chakula Barani Afrika kwa mujibu wa utabiri wa Malthus, tutazungumzia pia mgogoro wa chakula kwa Tanzania. Kutokua kwa kilimo na uzalishaji wa kilimo nchini na Barani Afrika kwa jumla kumesababisha tatizo kubwa la njaa kwa nchi nyingi, Tanzania ikiwamo. Karibu kila mwaka sehemu kubwa ya nchi Kusini mwa Afrika – maarufu kwa jina la nchi za Ushirikiano wa Kiuchumi Kusini mwa Afrika (SADC), ndizo zinazokumbwa zaidi na baa la njaa kutokana na matatizo mbalimbali, likiwamo la ukame.
Nchini Tanzania pekee, tatizo ni kubwa kiasi kwamba mara nyingi tumelazimika kuagiza chakula kutoka nje kwa fedha kidogo tuliyonayo na kwa njia ya kutembeza ‘bakuli la ombaomba’ ili kuokoa maisha ya wananchi ambapo wakati fulani tulifikia hatua ya kupokea tende kutoka Arabuni. Tatizo la chakula kwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Kiafrika linachangiwa kwa kiwango kikubwa na sera mbovu za kilimo na chakula.
Tunaweza kujiuliza; kwa nini tuwe na sera mbovu kwa sekta inayohudumia zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania? Tunakwenda wapi na ni nini ufumbuzi wa tatizo hili?
Mgogoro wa maendeleo ya kilimo nchini ni sehemu ya mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa kimataifa ambao chanzo chake kikuu ni pamoja na jinsi uchumi wake unavyojishirikisha na kuungana na uchumi wa dunia; uhusiano wa kibiashara usio sawa au kutoshabihiana na nchi za viwanda zilizoendelea; mgogoro katika mfumo wa kifedha wa dunia (world finance system) na kukosa nia njema kwa nchi za Magharibi ya kuwekeza katika maendeleo ya baadaye ya nchi zetu.
Tatizo la kilimo kwa nchi nyingi za Kiafrika (ikiwamo Tanzania), linaanzia karne ya 16 na kuendelea, ambapo nchi nyingi za Kiafrika
zilijiunga na mfumo wa uchumi wa kibepari wa dunia, kwa kuanzia na biashara ya utumwa ambayo ilitupunguzia idadi kubwa ya nguvu kazi kwa watu wengi kuuzwa nchi za nje.
Na ukoloni ulipoingia, uzalishaji wa chakula ulibezwa ambapo maeneo mazuri yalichukuliwa na wageni kwa kilimo kikubwa cha mazao ya biashara kama vile miwa, kahawa, chai na mengineyo liyoonekana kuinufaisha Ulaya. 

Uwekezaji binafsi na wa serikali uliegemea zaidi katika kuendeleza mazao hayo badala ya kuzalisha mazao ya chakula.
Hali hii inaendelea hadi leo chini ya sera za uchumi na soko huria zisizojali wengi (hasa wakulima wadogo wadogo) zinazosimamiwa na kushinikizwa kwetu na mashirika ya fedha, kama vile Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa madai kwamba huo ndiyo ukombozi pekee kwa tatizo la chakula nchini na kwa uchumi wa mkulima mdogo.
Mashirika hayo yanatuambia, maendeleo ya kiuchumi yatapatikana iwapo tu serikali itajiondoa katika kupanga uchumi (kwa manufaa ya watu wake) wala kujiingiza katika biashara na kuiacha nguvu ya soko itawale na kufanya kazi. Kitendo cha serikali kujitoa katika kupanga mipango ya uchumi yenye kumwendeleza mwananchi na kuacha nguvu ya soko ifanye kazi hiyo ni sawa na kumwacha mwananchi huyo amilikiwe na wenye mitaji, atumikishwe wapendavyo.
Mfano mzuri hapa kwetu ni ule mpango wa Kilimo cha Mkataba ulioandaliwa kutumika kwa wakulima wa pamba baada ya kushindwa vibaya kwenye kilimo cha tumbaku. Kwa mtazamo wa juu juu, mpango huu unaweza kuonekana mzuri lakini ukweli ni ndoano kwa mkulima mdogo aweze kuvuliwa kama samaki na wenye mitaji. Chini ya mpango huu, wakulima
wanatakiwa kuunda vikundi na kukopeshwa pembejeo za kilimo na mifuko ya kuvunia, kuingia mkataba na wakopeshaji wa kutomuuzia mtu mwingine mazao ila aliyewakopesha pekee, kutafutiwa mikopo ya benki, kulimiwa kwa mkopo ili kurejesha mikopo hiyo kwa kukatwa kwenye mauzo.
Dhamana ya mikopo hii ni ardhi ya mkulima iwapo atashindwa kurejesha mkopo kutokana na mazao atakayouza. Haijalishi mkulima huyo amekumbana na changamoto gani – ukame, mafuriko, mbegu kutoota na mengine kwa kuwa hana bima ya mazao.
Hapa, kuna maswali mengi kuliko majibu; ni nani anayepanga bei ya pembejeo katika soko huria? Ni nani anayepanga bei ya mazao kumpa mkulima bei nzuri kuweza kurejesha mkopo?  Bila shaka ni yule mwenye mtaji, ndiye anayepanga kwa misingi ya nguvu ya soko na kwa kuwa mkulima huyo atakuwa amebanwa kwa mkataba, kutouza mazao yake kwa mtu mwingine, tayari atakuwa mateka wa mwenye mtaji.
Ni mkulima gani mdogo anayeweza kuhimili masharti ya mabenki ya kigeni pamoja na riba, kama si kumfilisi? Mikataba gani hii isiyotambua majanga kama vile ukame, mafuriko na mengineyo ila kaulimbiu tu ya ‘lima, uza na kulipa’ kana kwamba mkulima huyo anaishi bustani ya Eden pasipo na majanga?
Mkulima gani mdogo anayeweza kuhimili kilimo cha trekta cha mkopo katika zama hizi, kama si kumwingiza katika deni lisilolipika?
Tunakosea kwa kudhani kwamba mkulima mdogo anaweza kuendelezwa badala ya kumwekea mazingira mazuri ya kujiendeleza. Kinyume chake ni ubeberu mpya katika kilimo utakaomrejesha kwenye maisha ya ki-manamba.
Soko huria na sera za ubinafsishaji haziwezi kuondoa matatizo ya kilimo na ya kiuchumi yanayotukabili leo kutokana na ukweli kwamba si mipango shirikishi. Badala ya kuwashirikisha wadau wa maendeleo ya nchi (wananchi) katika uamuzi, ‘wataalamu’ wa Ki-magharibi na watetezi wa sera za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wanatenda kivyao kwa kujiaminisha kuwa wanayajua matatizo ya wananchi. Matokeo ya yote hayo ni mipango isiyolenga kutatua matatizo wala kukidhi mahitaji, matakwa na matarajio ya watu.
Mawakala wa sera mbovu zinazosababisha baa la njaa sasa ni wasomi wetu nchini kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa na serikali za nchi za Magharibi (zenye kutoa misaada yenye masharti) na asasi za kimataifa.
Hawa wote wanaunda ‘muungano wa kisomi wa kimataifa’ (transnational elite coalition) ambao staili ya maisha, mahitaji na matashi yao ni tofauti na umma wa vijijini unaozalisha sehemu kubwa ya chakula. Ni ‘muungano’ huo wa kisomi uliodidimiza maendeleo ya kilimo nchini na sehemu nyingine nyingi Barani Afrika.
Muungano huu wa kitabaka ulianza muda mfupi tu baada ya uhuru, wakati nchi nyingi za Kiafrika zilipoiga kutoka nje mipango ya maendeleo iliyoabudu na kusisitiza uuzaji nje bidhaa pekee za kilimo na uanzishaji wa viwanda vya kati vyenye kutegemea fedha, nyenzo za kilimo na teknolojia kutoka nje.
Mipango hii ya muda mfupi ilikuwa ni kwa manufaa ya wasomi wachache nchini na rafiki zao wa nje na ambayo sasa imefilisi na inaendelea kufilisi uchumi wa nchi nyingi. Ni muungano huo hatari wa kisomi
ambao mpaka sasa unaendelea kuelekeza mipango na misaada ya kilimo kwenye mazao ya biashara, kwa manufaa ya asasi kubwa za kibiashara ndani na nje ya nchi na kubeza maendeleo ya kilimo cha mazao ya chakula.
Ni nani aliyeua viwanda vyetu vya msingi vya ndani vya enzi ya serikali ya awamu ya kwanza, vilivyolenga kumwendeleza mkulima mdogo? Nani aliua viwanda vya zana za kilimo – Ubungo (Kizaku) na Mbeya, kama si wasomi wetu kwa kushirikiana na wenzao wa kimataifa ili kuruhusu bidhaa za kigeni kufurika katika soko letu la ndani?.
Nani amebinafsisha benki zetu (NBC na CRDB) zilizokuwa na uso wa kibinadamu na kutuletea benki za kinyang’au, kama si wasomi wetu kwa kushirikiana na mawakala wa nje wa ukoloni mamboleo?.
Tatizo katika mgogoro wa chakula ni kwa wakulima wadogo wadogo kukosa umoja kuweza kuunda nguvu ya kisiasa. Hadi hapo wakulima watakapounda nguvu yao kuweza kutetea sera zenye manufaa kwao na kushinikiza matakwa yao kulingana na uwingi wao, wataendelea kuwa vikorombwezo tu ndani ya mfumo unaotawaliwa na wasomi wasio wa tabaka lao na matajiri.
Nani aliua viwanda vyetu vya kati; Sido na Kilimanjaro Machine Tools (KML), kama si muungano huo wa kisomi wa kimataifa na kuipokonya nchi yetu teknolojia ya kati ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kilimo?  Kwa nini leo sera zetu za uwekezaji hazizungumzii uwekezaji katika viwanda na teknolojia kama si njama za kuangamiza kilimo na kuendeleza baa la njaa? Wakulima wadogo wadogo ambao ndio wazalishaji wakubwa wa chakula wanahitaji mengi zaidi ya ardhi, mbegu, mbolea na pembejeo zingine; wanahitaji miundombinu ya kisiasa na mafunzo.
Mipango ya Kimagharibi na ya kisomi ya kuleta ‘mapinduzi ya kijani’ katika kilimo (green revolution) kwa teknolojia ya kisasa na kwa njia ya kilimo cha mashamba makubwa, mbegu za kisasa zinazotengenezwa katika maabara, matumizi ya mbolea za viwanda na mafuta, haiwezi kuondoa baa la njaa katika nchi masikini kama yetu; wala haiwezi kumwendeleza mkulima isipokuwa kumuuza utumwani ndani ya nchi ambayo serikali yake imejiondoa katika kupanga uchumi na maendeleo kwa ajili ya wanyonge hao.
Njia pekee ya kupambana na baa la njaa ni kumwendeleza mkulima mdogo kwa kuanzia na nyenzo na teknolojia ya kati, rahisi anayoweza kuimudu kiuchumi mahali alipo. Lazima tubadilike kwa kuweka mkazo juu ya
maendeleo vijijini badala ya kukazania maendeleo ya ‘vitu’ mijini, ubinafsishaji na uwekezaji usiojali na usioweza kuisaidia sekta ya
kilimo, hususan kilimo cha mkulima mdogo.
Hatuhitaji kukumbushwa juu ya mafanikio katika uzalishaji chakula miaka ya 1970, ambapo bila ya kupumbazwa na sera potofu za mapinduzi ya kilimo ya kijani za WB na IMF, Tanzania iliweza kuwahamasisha wakulima wadogo wadogo kuongeza uzalishaji wa chakula kwa mpango maalumu chini ya sera iliyodumu kwa muda mfupi ya ‘Kilimo cha Kufa na Kupona’ ambapo mwisho wa yote tuliweza kuzalisha chakula zaidi ya mahitaji ya nchi kwa mshangao wa wasomi na ndugu zao wa WB na IMF.
Matokeo mazuri kama hayo yalipatikana pia nchini Ghana miaka ya 1960, chini ya mpango wa ‘Operation Feed Yourself’ (Operesheni Jilishe), lakini punde tu ‘muungano wa kisomi wa kimataifa’ ulipobaini mafanikio hayo ya Ghana, uliihujumu sera hiyo na kufanya nchi kuwa tegemezi kwa chakula.
Muungano mkongwe kati ya nchi za Magharibi na wasomi wa nchi zetu, umeshindwa kuleta maendeleo na demokrasia. Hapa lazima tutafute dawa.
Tunatakiwa kuachana na watunga sera za kisomi wanaoabudu sera za Kimagharibi na kuweka watunga sera wawakilishi halisi wa walio wengi.
Tunataka maendeleo ya uchumi yawe mikononi mwa wengi, kwa kuwa ufumbuzi kwa tatizo la chakula na kilimo kwa jumla, ama utatoka kwa watu wenyewe au hautapatikana kabisa.  Tukumbuke ukweli kwamba hapajatokea watu kuwaponya wengine kwa hiari, badala ya kujiponya wao wenyewe; si hapo kale, wala si leo. 


Imeandikwa na Joseph Mihangwa

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου