Iran Swahili Radio, Alkhamisi, 30 Julai 2015
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umeelezea wasi wasi mkubwa ulionao kutokana na kuendelea vitendo vya utumiaji mabavu vya kundi la Boko Haram ambavyo vimepelekea mamia ya maelfu ya watoto nchini Nigeria kuwa wakimbizi. Ripoti ya UNICEF iliyotolewa Jumanne ya jana imeeleza kuwa, mashambulio na vitendo vya utumiaji mabavu vya Boko Haram katika miaka ya hivi karibuni vimepelekea watoto zaidi ya laki nane wa Nigeria kuwa wakimbizi. Ripoti hiyo inasema, akthari ya watoto hao wamelazimishwa kuolewa au wamebakwa.
Takwimu za hivi karibuni za Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita idadi ya watoto ambao ni wakimbizi nchini Nigeria imeongezeka maradufu. Wakimbizi wa Kinigeria wamekuwa wakikimbilia katika nchi za Chad, Cameroon na Niger ambazo zenyewe ni miongoni mwa nchi masikini duniani na hivyo kutokuwa na uwezo wa kuwalinda au kutoa huduma muhimu kwa wakimbizi hao. Ripoti zinaonesha kuwa, hata wanawake na watoto walioko katika kambi na vituo vya kimataifa vya Umoja wa Mataifa katika maeneo ya mpakani hawako salama.
Tangu kundi la Boko Haram lianzishe mashambulio yake nchini Nigeria hadi sasa zaidi ya raia milioni mbili wamelazimika kuyaacha makazi yao na kuwa wakimbizi. Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, jinai dhidi ya wanawake na watoto nchini Nigeria na katika nchi jirani na nchi hiyo ambazo zinashuhudia harakati za Boko Haram zimekuwa zikiendelea kufanyika. Siku chache zilizopita Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ulitangaza kuwa, kwa akali asilimia 75 ya mashambulio ya kujitolea muhanga yaliyotekelezwa nchini Nigeria mwaka huu yamefanywa na wanawake na watoto. Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo ni kuwa, katika miezi mitano ya awali ya mwaka huu, takribani mashambulio 27 ya kujilipua yalifanyika nchini Nigeria huku 9 kati ya hayo yakiwa yametekelezwa na watoto wenye umri wa kati ya miaka 7 na 17. Wanawake na watoto hao wamekuwa wakitekeleza mashambulio hayo ya kujilipua baada ya kupikwa kifikra na wanamgambo wa Boko Haram wakati wakishikiliwa mateka.
Hata kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameelezea kusikitishwa kwake katika taarifa mbalimbali alizotoa kuhusiana na kupanuka wigo wa mashambulio ya Boko Haram katika nchi za Kiafrika, kuongezeka utekaji nyara watu, kubakwa wanawake na mabinti na kutumiwa watoto kama mabomu ya watu, lakini pamoja na hayo hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa na Umoja wa Matifa kwa ajili ya kukabiliana na hali hiyo mbaya. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, baada ya kuingia madarakani Rais Muhammadu Buhari nchini Nigeria kulijitokeza matumaini ya kuokolewa nchi hiyo na raia wake kutoka mikononi mwa jinamizi la mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram, lakini baada ya kupita miezi miwili tangu aingie madarakani kiongozi huyo, wimbi la mashambulio ya Boko Haram limeshadidi na inaonekana kuwa, viongozi wa kimataifa ambao walipaswa kumsaidia Buhari na waitifaki wake katika kupambana na kundi hilo la kigaidi na kurejesha utulivu nchini Nigeria, hawana msaada mwingine ghairi ya kuonyesha masikitiko yao tu kuhusiana na hali hiyo.
Δεν υπάρχουν σχόλια:
Δημοσίευση σχολίου