Παρασκευή 9 Οκτωβρίου 2015

Utatu Mtakatifu, Mungu ambaye anapenda ubinadamu



Picha takatifu inayodokeza fumbo la Utatu kwa kuchora malaika watatu waliolakiwa na Abrahamu huko Mambre. Ilichorwa na mmonaki mtakatifu Andrej Rublëv (1360-1427) na kwa sasa inatunzwa Moscow, Tretjakow Gallery. 

*****
Sw.wikipedia (na hapa, hara, hapa & hapa)

Utatu au Utatu mtakatifu ni hali ya kuwa Watatu katika umoja kamili.
Jina hilo la ki teolojia linatumika hasa kufafanulia imani ya Wakristo wengi kwamba Mungu pekee, sahili kabisa, ni Nafsi tatu zisizotenganika kamwe: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

 
Mungu Baba ni nafsi ya kwanza ya Mungu katika imani ya Ukristo (isipokuwa Wasiosadiki Utatu)
Katika Uyahudi Mungu aliitwa pengine Baba kwa jinsi alivyo asili ya uhai na anavyoshughulikia watu wake, hasa Waisraeli, mfalme wao na mafukara, wanaopaswa kumtegemea kama watoto.
Kumbe katika Agano Jipya yeye ni hasa Baba wa Yesu, anayejitambulisha kama Mwana pekee wa Mungu. Nafsi hizo mbili pamoja na Roho Mtakatifu zinasadikiwa kuwa Mungu mmoja tu, asiyegawanyika katu.
Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli tangu mwaka 325 inafafanua kuwa Yesu Kristo "amezaliwa na Baba tangu milele yote", yaani si uzazi uliotokea wakati wowote wala mahali popote duniani. Daima Mungu Baba ni Baba wa Mwana, asingeweza kuwepo bila kumzaa Mwana.
Wakristo wanafurahia kushirikishwa uhusiano huo wa milele kwa kufanywa na Roho Mtakatifu (Gal 4:4) "wana ndani ya Mwana pekee": ndiyo maana ya kujiita "wana wa kambo" wa Mungu, wakati Yesu ni Mwana asilia.

Kwa agizo la Yesu watakaomuamini wanatakiwa kubatizwa kwa jina la hao watatu (Injili ya Mathayo 28:19). Agizo hilo la mwisho lilifuata na kujumlisha mafundisho yake mbalimbali kuhusu Baba, kuhusu yeye mwenyewe kama Mwana na kuhusu Roho Mtakatifu. 

Mwana wa Mungu - Yesu Kristo, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu  
Yesu alikuwa Myahudi mwanamume aliyeishi miaka 2000 hivi iliyopita (labda 6 KK - 30 B.K.).
Zaidi ya nusu ya wanadamu wote wanamuamini kuwa Mwana wa Mungu (wanaoitwa Wakristo) au walau nabii (hasa Waislamu).
Mafundisho yake yalilingana na yale ya Mafarisayo kuliko na yale ya Masadukayo, lakini alishindana pia na hao wa kwanza. Kijicho na upinzani vikazidi hasa Yerusalemu, walipoanza kufanya njama za kumuua. Ingawa Yesu alijua hayo, alijikaza kwenda katika mji mtakatifu autangazie habari njema na kufia huko.
Baada ya kupokewa kwa shangwe kabla ya sherehe ya Pasaka ya mwaka 30 (au 33) akakamatwa na baraza la Israeli kwa tuhuma ya kufuru ya kujilinganisha na Mungu, halafu akakabidhiwa kwa liwali wa Kirumi aliyekuwa na mamlaka ya kutoa adhabu ya kifo.
Baada ya kikao ambapo Wayahudi walitafuta kisingizio cha kisiasa, Ponsyo Pilato akalazimika kuagiza Yesu asulubiwe, na kisha kufa kwake kaburi lilindwe na askari. Hata hivyo siku ya tatu kaburi likaonekana tupu, na Yesu akaanza kuwatokea wanafunzi wake wa kike na wa kiume kwa muda wa siku arubaini, halafu akapaa mbinguni mbele ya macho yao.
Habari hizo zikatangazwa kwa sauti tu kwa miaka kadhaa, halafu zikaanza kuandikwa. Kanisa linaheshimu kwa namna ya pekee, kama ushuhuda mkuu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu na kama moyo wa Maandiko matakatifu yote, Injili nne zilizoandikwa na Marko, Mathayo, Mwinjili Luka na Yohane kati ya mwaka 65 na 100 hivi.



Sala zake

(Math 11:25-26)

Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako

(Yoh 11:41-42)

Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.

(Yoh 17:1-26)

Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako, na ulimwengu umewachukia, kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako, hao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo, ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.

Waumini wake wanaunda Kanisa la Kikristo. Wanamwamini kuwa Mungu aliyechukua umbile la mwanadamu au, kwa lugha nyingine, kuwa Mwana wa Mungu.



Roho Mtakatifu akionekana Kama Njiwa, katika Ubatizo wa Kristo.
 
Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu.

Jina

Kwa Kiebrania רוח ("ruah") ni jina la kike linalomaanisha roho, lakini pia upepo, pumzi. "Roho Mtakatifu" ni רוח הקודש, "ruah hakodesh".
Vilevile kwa Kigiriki neno ni "πνευμα" ("Pneuma"; kutokana na "πνεω", "pneō", yaani "kupumua/kupuliza/kuwa hai").
Kwa Wayahudi jina hilo linataja Nguvu za Mungu zinazoweza kujaza watu (kwa mfano manabii.
Wazo hilo lilistawishwa na Waeseni, halafu na Yohane Mbatizaji na Yesu Kristo.
 

Mifano

Kwa kuwa Nafsi ya tatu ni fumbo gumu kueleweka kuliko mengine, Biblia inamfananisha na vitu mbalimbali: maji, mpako, moto, wingu, mwanga, mhuri, mkono, kidole, njiwa.
 

Katika Agano la Kale

Tangu ukurasa wa kwanza wa Biblia ya Kiebrania uwepo wa Roho wa Mungu unatajwa kuhusu uumbaji wa ulimwengu


Katika Agano Jipya


Humo Roho Mtakatifu anafunuliwa na Yesu kikamilifu.
Ni hasa Injili ya Yohane (7:37-39; 14:16-17; 14:26; 15:7,26) inayomtambulisha kama παρακλητος, (kwa Kigiriki, paracletos), yaani Nafsi ambaye baada ya Yesu kupaa mbinguni anafariji/anatetea/anasimamia waamini badala yake.
Lakini hata Injili Ndugu, hasa Injili ya Luka, zinaonyesha uhusiano wa Roho Mtakatifu na Kristo tangu mwanzo wa maisha yake, yaani kuanzia umwilisho (Mt 1:18; Lk 1:34-35), kwa kupitia ubatizo (Mt 3:13-17; Mk 1:9-11; Lk 3:21-22; Yoh 1:31-33), miujiza (Mt 12:15-21; Mt 12:28; Mk 3:22-30) hadi kifo cha msalabani (Mt 27:50; Mk 15:37; Lk 23:46; Yoh 19:30).
Baada ya Yesu kumtoa kwa Bikira Maria, Mtume Yohane na wengineo wakati wa kufa na baada ya yeye kuwavuvia mitume wake jioni ya Pasaka ya ufufuko, Roho Mtakatifu alidhihirika kwa kishindo kwenye Pentekoste ya mwaka ule (Mdo 2:1-11), haohao na wengineo walipokuwa wakimngojea wakisali kwa umoja.
Hapo Mtume Petro na wenzake walianza kutangaza habari njema kwa watu wa lugha mbalimbali waliokuwa Yerusalemu kwa ajili ya hija


Vipaji vya Roho Mtakatifu 

 
Mapokeo ya Kikristo, yakitumia Isa 11:2, yanaorodhesha vipaji saba vinavyoombwa hasa wakati wa kipaimara: hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji wa Mungu.
Kwa vipaji hivyo Roho Mtakatifu anamuongoza kila mmoja katika safari ya kumfuata Kristo hadi kuchuma yale yanayoitwa na Mtume Paulo matunda ya Roho Mtakatifu: "upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi" (Gal 5:22).
Tofauti na vipaji na matunda ni karama mbalimbali ambazo Roho Mtakatifu anazigawa anavyotaka kwa ujenzi wa Kanisa: karama yoyote si ya lazima kwa wokovu wa mtu, wala hailengi kwanza utakatifu wake, bali faida ya wengine.


Yesu Kristo
 
Wasiosadiki Utatu
 
Biblia haitumii neno Utatu, ambalo limetungwa na wanateolojia katika jitihada za kufafanua ukweli wa Yesu Kristo kama Mwana wa Mungu na wa Roho Mtakatifu.
Kwa kuwatambua wote wawili kuwa wa milele lakini si Baba, wanateolojia wengi, hasa mababu wa Kanisa, walikiri kuwa zote tatu ni nafsi tofauti za Mungu pekee.
Mitaguso ya kiekumene kuanzia karne ya 4 ilithibitisha mafundisho hayo kama imani sahihi na kutupilia mbali yaliyo kinyume kama uzushi.
Hata hivyo Waario na wengineo hawakukubali dogma hizo, hivyo asilimia ndogo ya Wakristo imeendelea kukataa kusadiki fumbo la Utatu, na kukiri umoja wa nafsi ya Mungu, ingawa kwa kutofautiana wao kwa wao.
Kati ya makundi makubwa zaidi yenye msimamo huo kuna Wamormoni na Mashahidi wa Yehova, lakini pia baadhi ya Wapentekoste.

 

Utatu Mtakatifu - Ufafanuzi wa teolojia

Umoja wa Nafsi hizo unatokana na asili yake pekee, yaani Baba ambaye ndani mwake anamzaa milele Mwana kama mwanga toka kwa mwanga, kama Neno au Wazo lake (Hekima), tena anamvuvia Roho Mtakatifu kama Upendo ambao unamuunganisha na Mwana na kukamilisha umoja wao.
Kimsingi ni kwamba Mungu pekee (Baba) anajifahamu milele (Mwana) na kwa kujifahamu anajipenda (Roho Mtakatifu). 


Katika matamko rasmi ya Kanisa

Imani hiyo ilizidi kufafanuliwa hasa katika karne IV, mitaguso mikuu ya kwanza ilipochukua msimamo dhidi ya wazushi waliokanusha umungu wa Yesu na wa Roho Mtakatifu. Ilipata muundo wa kudumu katika Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli inayotumika hadi leo katika madhehebu mengi ya Ukristo.
 

Katika liturujia

Fumbo hilo linaadhimishwa katika liturujia ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo wa mashariki (siku ya Pentekoste) na ya Ukristo wa magharibi (Jumapili inayofuata).


Ona pia
God the Holy Trinity: ‘The Lover of Mankind’ (& the "depiction of God" in Orthodox Church)
Kanisa la Orthodox na Kanisa Katoliki 
Liturghia Takatifu
Maaskofu Orthodox watakatifu watatu: Basili Mkuu, Yohane Krisostomo na Gregori wa Nazianzo 

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου