African Brotherhood Foundation
Picha hapa |
Mtazamo wa African Brotherhood Foundation, kama ilivyo siku zote katika dunia, mungu ameumba vitu mbalimbali kwa maana yake. Leo hii kona ya ABF Africa imeona igusie na kuelezea juu ya mwanamke. Kimantiki ndani ya dunia hakuna mwanadamu asiye zaliwa na mwanamke na watu wote ni lazima tuwathamini wanawake. Sifa za mwanamke katu hatuwezi kuzimaliza kwa maana thamani yake ni kubwa na zenye kuvutia ukizisikiliza na kuziona. Katika bara letu la Afrika wanawake wana mchango mkubwa sana. Busara zao ndizo zilichangia Afrika kuwa huru mpaka hivi sasa ingawa wadai uhuru wa nchi nyingi za Afrika walikuwa ni wanaume. Lakini ukitazama utaona mwanamke alikuwa nyuma ya mwanaume kwa kumpa mawazo na muelekeo mzuri ndio maana mambo yalikwenda kwa kasi na uweledi kwasababu kama tunavyo jua mwanamke akilala jamii imelala.
Hebu tazama mwanamke alivyokuwa mbunifu. Familia nyingi za bara hili la afrika zinategemea uwepo wa mwanamke ili ziweze kupata maendeleo ya mali, chakula na hata mavazi. Hii ni kwa sababu yeye ndiye chanzo cha ufanisi katika jamii kwenye kutimiza wajibu wa kila siku. Mungu aliwaumba kwa makusudio maalumu ya kuisaidia na kuikomboa jamii sio kuwa wasindikizaji kama madai ya baadhi ya watu wenye fikra potofu na mawazo mgando. Kona ya ABF Africa inapenda kuwaambia watu wanaonyanyasa wanawake waache mara moja, hivi nyie hamna huruma wala chembe ya ubinadamu hata kidogo? Mama amebeba ujazito wako miezi tisa, amejifungua kwa uchungu na kukulea kwa shida na dhiki na kufikia kipindi chakula nyumbani hakuna aliweza kutumia maarifa ya ziada kwa kuchemsha mawe ili akupe moyo na kutuliza njaa yako? Vilevile kufanya jitihada kwa kupata chakula kwa siku inayo fuata iwe kwa kukopa au njia nyingine lakini leo hii wewe binadamu usiye na huruma wala shukurani kwa mwanamke unamdharau na kumnyanyasa! Tambua amani unayo iona hii imetokana na yeye kwa sababu ndiye chanzo cha amani duniani kwa ujumla kutokana analeta utulivu na kuzuia jazba za kina baba majumbani. Leo sisi ni mashuhuda viongozi wengi wanapendeza na kupanda majukwaani na kujinasibu ni kazi kubwa inayofanywa na wanawake kwa utashi mkubwa waliopewa na mungu.
Asiye mpenda mwanamke asipewe kipaumbele cha aina yeyote ile katika jamii, ushujaa wa mwanamke upo kwenye mafungu yote ya kinadharia na kivitendo. Mtazamo wa kona ya ABF Afrika ni kuona Afrika inaungana ili kukata kiu kubwa ya watu wengi wa bara letu. Hii ndio maana imeamua kumuelezea mwanamke kwa kutambua kabisa bila ya yeye kuwepo na kushirikishwa muungano tunao upigania hauwezi kupatikana bila michango yao. Na kwa kulifahamu hilo ni lazima tuwashirikishe moja kwa moja na kuungana nao kwenye harakati zao zote za mabadiliko kimaneno na vitendo.
Maasai, Kenya (hapa na hapa)
Jamii za kiafrika zinapaswa zibadilike ili ziweze kupata maendeleo vilevile zitambue kwenye kila jambo la kimaendeleo kuna mwanamke, kona ya ABF Afrika itaendelea kulaani mateso, ukandamizaji, ukatili na unyanyasaji dhidi ya mwanamke bila ya kificho wala uwoga wa aina yeyote. Kama taasisi changa ya AFRICAN BROTHERHOOD FOUNDATION (ABF) kwa pamoja tunatambua mchango mkubwa unaofanywa na mwanamke, huu sio wakati wa kulalamika, mtumie fursa za kujenga hoja zenye mantiki na zenye kuleta mabadiliko kwenye jamii za kiafrika. Kwa maana hiyo kushirikiana na mwanamke kutaleta misingi ya uzalendo, utawala bora, umoja na mshikamano wa hali ya juu kwa bara la Afrika.
Vilevile tunatambua michango iliyofanywa na inayofanywa na wanawake katika bara hili shukrani kubwa kwa marehemu Bibi TITI MOHAMED, Mama MARIA NYERERE, Mama GRACE MACHEL, Mama WINNIE MADIKIZZELA MANDELA , Mama SALMA KIKWETE, HELLEN SELIF JOHNSON, DKT. ASHA ROSE MIGIRO, PROF ANNA TIBAIJUKA na wengine wote kwa michango yao iliyotupelekea tupate uhuru na maendeleo ya bara la afrika. Wanawake wote hawapaswi kukata tamaa, wanapaswa kuongeza juhudi na kuunganisha maarifa yao kwa pamoja wataleta maendeleo endelevu na kulifanya bara la afrika kwenda mbele.
Wito wetu kwenu ni kuwaasa mtumie nafasi mnazo zipata kudumisha umoja wenu pamoja na ule wa Afrika, tusisubiri maadhimisho ya kila mwaka bali tushirikiane pamoja kila wakati na kupambana na wale wote wasio watakia mema. Ni vyema kupambana nao kwa sheria ili iweze kuwa fundisho kwa wale wanao wanyanyasa wanawake na kuwanyima haki zao za msingi. Kuliko kuwaacha na kuzidi kuwafanyia wanawake matendo maovu yasio stahili katika jamii na kuzidi kuwarudisha nyuma.
Vilevile kwa upande wa serikali za Afrika zitazame kwa umakini sekta ya afya hususani kwa upande wa wodi za wazazi. Hospitali nyingi hazina vifaa vya kutosha ukiangalia kitanda kimoja utakuta watu zaidi ya mmoja hii ina hatarisha afya ya mama na mtoto hebu tuwe na chembe ya huruma kwa hawa mama zetu, bila ya wao tusinge kuwa hapa tulipo na jamii yeyote bila ya mwanamke haiwezi kuendelea.
Serikali ina wajibu wa kutunga sheria itakayo mlinda mwanamke na kumpa utambulisho katika jamii kutokana mila potofu zimekuwa zikimnyima haki za kimsingi kama vile kuzuiliwa kwenda shule, kutokuwa na maamuzi katika jamii. Hivyo basi ili kumsaidia mwanamke kuondokana na manyanyaso anayoyapata kila siku hakuna asiyejua kama mwanamke anaweza kufanya mabadiliko yaletayo tija na manufaa kwa jamii zetu tumeweza kuona baadhi yao na tuna mifano ya kuwazungumzia na kujivunia uwepo wao.
Christina Mothapo, Mamelodi (hapa)
Kuna umuhimu mkubwa wa kutungwa kwa sera ya kumlinda na kumtetea mwanamke. Ni jukumu la serikali na wadau kwa kushirikiana kwa pamoja. Hii itamuwezesha mwanamke kutoka kifungoni alipo kwa muda mrefu sasa bila ya hatia yeyote, hivi ni kosa kwa wao kuwepo duniani? Au wemepoteza uhalali wa kuishi? Maana tafsiri potofu za baadhi ya watu zimewafanya wanawake kuwa kama yatima waliokosa misaada ya kimaisha. AFRICAN BROTHERHOOD FOUNDATION (ABF) imeona “ni bora kufa kuliko kuishi na hisia zilizo kufa” kwa kulikemea hili kwa nguvu moja na kutangaza rasmi uadui na wale wote wanaomtesa na kumnyanyasa mwanamke na kuzitaka jamii zote za Afrika kushirikiana katika kumkomboa mwanake kwa nguvu moja.
Mwisho, wakati wa kusimamisha haki za wanawake umefika. Afrika ni mali ya watu wote. kuheshimiana na kuvumiliana itajenga jamii ya watu wenye fikra hai zenye mashiko ndipo maendeleo yatapatikana bila ya kupiga hodi wala foleni kwa kusubiri misaada kutoka ughaibuni. Mwanamke ndiye nguzo na mustakabali wa bara la Afrika na dunia kiujumla.
Ona pia
Bikira Maria, Mama wa Mungu
African Women
Mother of God (Virgin Mary), Orthodox Church and African peoples
Ethiopian Slave Girl Beaten By Saudi Family ?
Δεν υπάρχουν σχόλια:
Δημοσίευση σχολίου