Iran Swahili Radio, 29 Julai 2015
Rais Barack Obama wa Marekani jana baada ya adhuhuri
aliondoka Addis Ababa Ethiopia na kuelekea Washington na kwa utaratibu
kuhitimisha safari yake ya siku tano barani Afrika ambapo alizitembelea
Kenya na Ethiopia. Akihutubu katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, Rais
Obama alizungumzia uhusiano wenye uwiano na bara la Afrika, vita dhidi
ya ugaidi na demokrasia. Wakati Rais Obama alipoingia madarakani
wananchi wengi wa Afrika hususan watu wake wa karibu nchini Kenya
walifurahi sana. Walikuwa na matarajio makubwa na Rais huyo mwenye damu
ya Afrika, hata hivyo sera za Marekani barani Afrika ziliendelea kama
zilivyokuwa huko nyuma na hazikuwa na natija chanya na ya kuridhisha
kama vile amani kwa bara hilo.
Fauka ya hayo hatua ya Marekani ya
kuingilia mambo ya nchi nyingine iliandaa uwanja wa kutokea mivutano na
migogoro kwa makumi ya nchi za Kiafrika na hali hiyo kupelekea kutokea
vita kadhaa barani Afrika. Hatua za Marekani katika miaka ya hivi
karibuni barani Afrika zinaonesha kuwa, serikali ya Washington mbali na
kushindana kiuchumi na washindani wenzake kama China barani Afrika,
ilichukua hatua ya kupanua harakati zake za kijeshi katika bara hilo.
Kuasisiwa kikosi cha Marekani barani Afrika AFRICOM mwaka 2008 kwa
kisingizio cha kupambana na ugaidi ni jambo linalotathminiwa katika
uwanja huo. Katika hali ambayo kabla ya hapo vita vya siri vya Marekani
nchini Somalia, Yemen, Libya na Mali vilikuwa vimefichuliwa, hivi sasa
viongozi wa Marekani wametangaza wazi mpango wao wa kutuma wanajeshi wa
nchi hiyo kwa uchache katika nchi 35 za Kiafrika.
Jenerali Raymond
Odierno Mkuu wa Vikosi vya Marekani amesisitiza katika mahojiano
aliyofanyiwa na gazeti la Washington Times kwamba, kutumwa vikosi vya
Marekani kunafanyika katika fremu ya stratejia ya nchi hiyo ya kutuma
vikosi katika maeneo mbalimbali ya dunia ili ikilazimu iweze kuwa na
radiamali ya haraka ya kukabiliana na changamoto itakayojitokeza. Ukweli
wa mambo ni kuwa, viongozi wa Marekani wanaamini kuwa, bara la Afrika
limo katika hali ya kubadilika na kuwa la kiistratejia katika uga wa
kimataifa ambapo kuanzishwa vituo vya kijeshi barani humo ni miongoni
mwa malengo ya Washington ya kuwa na satuwa na udhibiti barani humo. Kwa
sasa kuna mamia ya wanajeshi wa Marekani nchini Niger. Nchini Chad pia
kuna vikosi vya Marekani ambavyo vimetumwa huko kwa kisingizio cha
ushirikiano wa kiusalama.
Nchi ya Somalia nayo ni moja ya walengwa wakuu
wa operesheni za kijeshi za Marekani yakiwemo mashambulio ya ndege
zisizo na rubani. Serikali ya Obama pia ilituma vikosi vya Marekani
katika nchi kadhaa za katikati na mashariki mwa Afrika mwaka 2011 kwa
kisingizio cha kufanya juhudi za kuwatia mbaroni viongozi wa kundi la
waasi wa LRA wa kaskazini mwa Uganda.
Vyombo vya Marekani vimesema kuwa,
Washington inataka kuanzisha kituo cha kijeshi cha ndege zisizo na
rubani nchini Niger au Burkina Faso ili kupitia kituo hicho iweze
kuongoza operesheni za kijasusi kaskazini mwa Afrika. Kambi ya kijeshi
ya Lemonnier ya Marekani nchini Djibouti nayo imo katika hali ya
kupanuliwa na idadi ya wanajeshi wa Kimarekani walioko katika kambi hiyo
wameongezeka. Hapana shaka kuwa, madai ya Marekani ya kupambana na
ugaidi yangali yanatumiwa kama wenzo wa Washington wa kupanua hatua zake
za kijeshi barani Afrika.
Δεν υπάρχουν σχόλια:
Δημοσίευση σχολίου