Παρασκευή 30 Οκτωβρίου 2015

'Kipindupindu chaweza kuenea hadi nje ya Tanzania'


Iran Swahili Radio

'Kipindupindu chaweza kuenea hadi nje ya Tanzania'Shirika la Afya Duniani (WHO) limeionya Tanzania juu ya kuenea ugonjwa hatari wa kipindupindu nchini humo na kwamba ikiwa hatua za maana hazitochukuliwa, basi kuna uwezekano ugonjwa huo ukaenea hadi nchi jirani pia. Dominique Legros, mkuu wa kitengo cha kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu cha shirika hilo amesema kuwa, hadi sasa kuna kesi 5000 za maambukizi ya ugonjwa huo nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu mwezi Agosti mwaka huu hadi juzi tarehe 21 Oktoba, jumla ya kesi 4,922 za maambukizi ya kipindupindu zilikuwa tayari zimeripotiwa. Dominique Legros ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuzuia kuenea ugonjwa huo nchini Tanzania, ili kuzuia pia maambukizi hayo katika nchi jirani. Aidha mkuu huyo wa kitengo cha WHO cha kupambana na ugonjwa wa kipindupindu amesema kuwa, kukosekana maji salama ya kunywa, ndiyo sababu kuu ya kuenea kwa kasi ugonjwa wa kipindupindu nchini Tanzania. 
Mara ya mwisho kuenea ugonjwa wa kipindupindu katika eneo la Afrika Mashariki ilikuwa mwaka 1990, ambapo katika kipindi hicho karibu watu laki mbili waliambukizwa ugonjwa huo ndani ya nchi nne wanachama wa EAC, huku karibu watu wengine 8000 wakipoteza maisha.

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου