Sakramenti
(Nakala hii ina taarifa kutoka humo : Sw.wikipedia na maneno yangu mwenyewe)
Orthodox Ubatizo nchini Rwanda (hapa)
Sakramenti katika mapokeo na imani ya Ukristo ni ishara na chombo cha neema ya Mungu.
Jina hilo linatokana na neno la Kilatini "sacramentum" linalofanana na lile la Kigiriki "mysterion" (fumbo).
Ni mafumbo kwa kuwa ishara ya nje (vitendo na vitu vinavyosindikizwa na maneno maalumu) zinamletea mtu neema zisizoonekana.
Wakristo Orthodox wanasadiki zina uwezo huo bila ya kutegemea utakatifu au sifa nyingine ya mhudumu anayezitoa kwa mwamini.
Kwa ajili hiyo ni lazima sakramenti ziwe zimewekwa na Yesu Kristo ambaye alizikabidhi kwa Kanisa ili liendeleze kazi yake ya kutakasa binadamu.
Katika milenia ya kwanza, neno lilitumika kwa ibada yoyote. Kwa mfano, Agostino wa Hippo alisema Kanisa linaishi sakramenti nyinginyingi, akiorodhesha maji ya baraka, ndoa, ekaristi, mazishi n.k.
Baadaye jina likaja kutumika kwa namna ya pekee kutajia zile ibada zilizowekwa na Yesu mwenyewe, ingawa pengine linaendelea kutumia kwa maana pana ya "ishara na chombo". Kwa mfano, "Kanisa ni sakramenti ya umoja".
Sakramenti
Ubatizo
Kipaimara
Ekaristi
Kitubio
Mpako wa wagonjwa
Daraja takatifu
Ndoa
Kwa njia yake Yesu anaingia katika maisha ya binadamu ili kuwaunganisha naye hasa katika fumbo la Pasaka (yaani kifo na ufufuko wake).
Sakramenti tatu za kwanza ni za kumuingiza mtu katika Ukristo.
Sakramenti mbili zinazofuata ni za uponyaji wa roho na mwili.
Sakramenti mbili za mwisho ni za kuhudumia ushirika katika Kanisa na katika familia iliyo kanisa dogo.
Ubatizo (hapa)
Ubatizo ni sakramenti ya kwanza ya Ukristo. Unaitwa "mlango wa sakramenti", kwa sababu ni lazima kuupokea kabla ya kupokea nyingine yoyote, hasa ekaristi.
Sakramenti ya kwanza daima ni ubatizo, kwa kuwa ndio kupata uzima mpya kwa kushiriki kifo na ufufuko wa Yesu, inavyodokezwa wazi zaidi mtu akizamishwa na kutolewa majini. “Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima” (Rom 6:4). Sakramenti nyingine zote ama zinastawisha ama zinafufua uzima huo wa Kimungu ambao ni sharti la kuingia mbinguni. “Amin, Amin, nakuambia: Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu” (Yoh 3:5).
Jina
Orthodox Ubatizo katika Kananga (hapa)
Jina linatokana na kitenzi cha Kigiriki βαπτίζω (baptizo, maana yake nazamisha majini, naosha, lakini pia nanawa).
Maana ya kwanza inadokeza lengo la kumzika mtu ili afufuke pamoja na Yesu Kristo katika uzima mpya.
Maana ya pili na ya tatu zinadokeza lengo la kumtakasa mtu kutoka dhambi zake
Ibada zinazotumia maji zinapatikana katika dini nyingi, kutokana na kitu hicho kumaanisha wazi uzima na usafi.
Ubatizo unafanyika kwa maji kwa kuwa ndiyo ishara ya usafi na ya uhai unaotupatia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. “Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu” (Ez 36:26-27). “Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo” (Ufu 22:1).
Ubatizo unatolewa pia kwa maji machache tangu mwanzo wa Kanisa. Kutokana na umuhimu wa sakramenti hiyo Yesu ametuagiza twende kubatiza watu duniani kote. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaonyesha waamini walivyotekeleza agizo hilo katika mazingira mbalimbali, si tu yalipopatikana maji mengi. Hivyo Mtume Paulo alipokuwa ndani ya nyumba “akasimama akabatizwa” (Mdo 9:18). Kumbe Yohane Mbatizaji hakusogea mbali na mto Yordani, akisubiri watu wamuendee kutoka maeneo yote ya nchi ile kame. “Alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele” (Yoh 3:23).
Ubatizo wa Yohane
Ubatizo Yesu (hapa)
Yohane Mbatizaji alipotikisa Wayahudi wenzake kwa kuhubiri toba kandokando ya mto Yordani aliwadai wapokee "ubatizo wa maji" kama ishara ya kuongoka na ya kuwa tayari kumpokea Masiya ajaye, atakayebatiza "kwa Roho Mtakatifu na moto" (Math 3:11).
Ubatizo uliotolewa na Yohane Mbatizaji haukuwa sakramenti, kwa sababu yeye alikuwa mtangulizi tu wa Yesu, mwanzilishi wa sakramenti zote. “Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Math 3:11). Paulo aliuliza watu, “‘Mlibatizwa kwa ubatizo gani?’ Wakasema, ‘Kwa ubatizo wa Yohane’. Paulo akasema, ‘Yohane alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu’. Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu” (Mdo 19:3-5).
Tofauti kubwa kati ya ubatizo wa Yohane na ule wa Yesu ni kwamba sakramenti inategemea imani kwa Kristo na kutushirikisha kifo na ufufuko wake. “Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo” (Gal 3:27). Ndivyo inavyoondolea dhambi zote na kuingiza katika uzima wa Utatu Mtakatifu. Kwa sababu hiyo Yesu aliagiza tubatize “kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Math 28:19). Maneno hayo ndiyo muhimu zaidi katika sakramenti hiyo. Maji peke yake, hasa yakiwa mengi, yanaweza kuosha mwili, lakini si roho. Kumbe ubatizo unaotuokoa “siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu” (1Pet 3:21).
Ubatizo alioupokea Yesu
Yesu alibatizwa na Yohane akiwa na umri wa miaka 30 hivi akithibitisha ubora wa kazi ya mtangulizi wake na utayari wa kubeba dhambi za ulimwengu kama mwanakondoo wa sadaka ya upatanisho.
Hapo Roho Mtakatifu alimshukia kwa sura ya njiwa na Mungu Baba alimshuhudia kuwa ndiye Mwana wake mpendwa, aliyempendeza kwa utiifu wake (Mk 1:11). [Ona pia Utatu Mtakatifu, Mungu ambaye anapenda ubinadamu]
Ubatizo uliotolewa na Yesu
Injili ya Yohane inashuhudia kwamba Yesu pia alianza kubatiza, tena watu wengi kuliko Yohane, ingawa kwa njia ya wanafunzi wake (Yoh 3:22; 4:1-2).
Hasa ni baada ya kufufuka kwamba aliwaagiza wakabatize mataifa yote: "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu" (Math 28:19).
Orthodox Ubatizo katika Burundi (hapa)
Ubatizo wa watoto wachanga
Kadiri ya madhehebu mengi, watoto wachanga wanaweza kubatizwa kwa sababu hawakatai neema ya Mungu. Wanafunzi wa Yesu walipotaka kuwazuia wasiletwe kwake “alichukizwa sana, akawaambia, ‘Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni: Yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa” (Mk 10:14-15). Yeremia aliambiwa, “Kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yer 1:5). Yohane Mbatizaji alitabiriwa “atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye” (Lk 1:15).
Ingawa watoto wachanga hawawezi kuelewa kinachofanyika, Mungu anaweza kuwamiminia rohoni mwanga wa imani. “Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao umeiweka misingi ya nguvu” (Zab 8:2). “Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake... kwa shangwe” (Lk 1:41,44). “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako” (Math 11:25-26).
Hata watu wazima hawawezi kuelewa sakramenti kwa dhati, kwa kuwa zote ni mafumbo yanayotuzidi. Basi, kama Mtume Petro alipooshwa miguu, tumuachie Bwana atufanyie kazi anavyojua yeye. “Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye” (Yoh 13:7). Kisha kuoshwa tuzidi kuchimba mafumbo hayo kwa mwanga wa Neno na wa Roho Mtakatifu. “Je, mmeelewa na hayo niliyowatendea?... Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” (Yoh 13:12,15).
Kumbe, imani ya watu wazima inaweza kufaidisha watoto kama wengine pia. Walimletea Yesu “mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne... Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, ‘Mwanangu, umesamehewa dhambi zako” (Mk 2:5). Kwa ubatizo watoto wanaunganishwa naye na kuanza kuponywa madonda ya dhambi ya asili. “Tazama, mimi naliumbwa kati hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani” (Zab 51:5). “Ikiwa kwa kukosa mtu mmoja mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo” (Rom 5:19).
Ubatizo wa watoto wachanga unafanyika tangu mwanzo, usipingwe na yeyote kwa miaka elfu na zaidi. Ni kwamba Wayahudi walipokea watoto katika dini yao kwa kuwatahiri siku ya nane baada ya kuzaliwa. “Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu” (Lk 2:21). Watu wa mataifa walipoongokea dini hiyo, walioshwa na kutahiriwa pamoja na watoto wao. Mitume pia walipokea katika Kanisa familia nzima, si wazazi tu. Walibatizwa “yeye na nyumba yake”, “yeye na watu wake wote” (Mdo 16:15,33); “watu wa nyumbani mwa Stefana” (1Kor 1:16).
Ubatizo na sakramenti nyingine
Ubatizo hautoshi, bali unahitaji kukamilishwa na kipaimara na ekaristi, kama vile baada ya kuzaliwa tunahitaji kukomaa na kudumisha uhai wetu kwa chakula. Sakramenti hizo tatu kwa pamoja ni msingi wa maisha ya Wakristo wote, kumbe nyingine zinahitajika tu katika hali na nafasi maalumu. Mitume waliwaendea Wasamaria “wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana Yesu. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8:15-16). “Amin, amin, nawaambieni: Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu” (Yoh 6:53).
Wakristo Orthodox ambao tu waliobatizwa, Malawi (hapa)
Kipaimara (hapa)
Sakramenti inayohusiana zaidi na ubatizo ni kipaimara, kinachoendeleza kazi yake. “Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao” (Mdo 19:5-6). Sakramenti hizo ni kama pande mbili za pesa moja. Zinahusiana kama Pasaka na Pentekoste, ambayo ni utimilifu wake, kwa kuwa siku alipofufuka Yesu aliwapulizia Mitume Roho Mtakatifu, ambaye siku hamsini baadaye akawajia kama “upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote” (Mdo 2:2).
Kipaimara ni sakramenti ya pili katika safari ya kuingizwa katika Ukristo ambayo inaanza kwa Ubatizo na kukamilishwa na Ekaristi.
Ishara
Kwa kuwa hii ni hasa ibada ya Roho Mtakatifu, ishara yake ni tendo la kuwekea mkono kichwani, inayomaanisha kumuita juu ya mhusika.
Pamoja na kuwekea mikono na mwandamizi wa Mitume, ni lazima pia kupaka paji la uso kwa mafuta ya kunukia yanayoitwa "krisma") pamoja na kutamka maneno yanayoweka wazi kwamba ndiye anayetolewa kama paji na mhuri wa kuwa mali ya Bwana. Ndiyo inayowafanya watu waitwe Wakristo nyuma ya Yesu aliyeitwa Kristo. “Kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu” (Yoh 6:27). “Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu” (2Kor 1:21-22).
Madondoo mengine yanayozungumzia mpako na mafuta kuhusiana na Ubatizo ni 2Kor 1:21 na 1Yoh 2:20,27.
Picha hara
Neema ya kipaimara
Kumpokea Roho Mtakatifu maana yake ni kuja kuongozwa naye badala ya kutawaliwa na shetani. “Kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwetu, aliaye, ‘Aba!’ yaani, ‘Baba!’ Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu. Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu... Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho” (Gal 4:6-8; 5:25). “Ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake” (Rom 8:9).
Tukimpokea Roho Mtakatifu papo hapo tunapokea pia adili kuu la upendo: “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Rom 5:5). Tena tunapokea vipaji vyake ambavyo Yesu alikuwa navyo kikamilifu. “Roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana. Na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana” (Isa 11:2-3). Mambo hayo, tofauti na karama, ni ya lazima kwa yeyote apate wokovu wa milele.
Tunda la kuongozwa na Roho Mtakatifu ni umoja wa Kanisa unaotokana na ustawi wa upendo na vipaji ndani ya waamini. “Wote walijaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja” (Mdo 4:31-32). “Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria” (Gal 5:22-23). “Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi, ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi; tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki” (Yak 3:14-17).
Ekaristi (hapa)
Jina linatokana na neno la lugha ya Kigiriki εὐχαρίστω (eukharisto: nashukuru) lililotumiwa na Mtume Paulo na Wainjili katika kusimulia karamu hiyo ya mwisho ya Yesu na Mitume wake, na muujiza uliotangulia ambao Yesu alidokeza nia yake ya kushibisha binadamu wote, yaani ule wa kuzidisha mkate na samaki kwa ajili ya umati.
Jina linaonyesha mazingira ya sala ya matukio hayo, ambapo Yesu alimuelekea Mungu akimshukuru kwa vyakula na kinywaji alivyoshika mikononi kabla hajawagawia wanafunzi.
Shukrani ilikuwa msimamo wa msingi wa Yesu kwa Baba maisha yake yote, hasa alipofikia wakati wa kutolewa awe kafara ya wokovu wetu. “Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, ‘Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu’. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, ‘Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu’” (1Kor 11:23-25).
Mkate na divai
Ortodox Mkristo Liturujia takatifu katika Kasoa, Ghana
(hapa, kuangalia video hapa na hapa - Zambia)
Yesu alitumia mkate na divai kwa sababu vilikuwa vya maana sana katika utamaduni wake na katika Agano la Kale. Vilikuwa chakula cha kawaida na kinywaji cha karamu. “Divai imfurahishe mtu moyo wake... na mkate umburudishe mtu moyo wake” (Zab 104:15). Vilitokana na chembe za ngano na matunda ya mzabibu ambavyo Yesu alijifananisha navyo. “Amin, amin, nawaambia: Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yoh 12:24). “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yoh 15:5). Baada ya kulimwa, vilihitaji kusagwa au kushinikizwa, matendo yanayodokeza tena mateso yake pamoja na kazi ya binadamu. Pia wingi wa chembe na wa zabibu zinazoungana ziwe mkate na divai unamaanisha umoja wa waamini ndani ya Kristo. Kwa hiyo ni lazima tutumie daima mkate na divai, si vitu vingine.
Yesu mwenyewe alizungumzia mkate kuliko divai, kwa sababu chakula ni muhimu kuliko kileo. “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu” (Yoh 6:51). “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (1Kor 10:17). Anayekula umbo la mkate hapokei sehemu tu ya Yesu, bali anampokea mzima, Mwili, Damu, Roho na Umungu. Pamoja na hayo, daima ni lazima walau padri anywe umbo la divai.
“Melkizedeki mfalme wa Salemu alileta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu aliye juu sana” (Mwa 14:18), “amefananishwa na Mwana wa Mungu” (Eb 3:7). “Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana” (Isa 25:6). “Njoo, ule mkate wangu, ukanywe divai niliyoichanganya” (Mith 9:5-6). Yesu alishiriki karamu nyingi na katika mojawapo ndipo alipoanza miujiza yake kwa kugeuza mapipa ya maji kuwa divai bora. “Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa” (Yoh 2:10). “Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa, nanyi mwasema, ‘Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi” (Lk 7:34).
Hatimaye Yesu alitumia divai kuachia ishara ya damu yake ili wafuasi wake waweze kushiriki mateso yake. “Je, mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi?” (Math 20:22). Kisha kushiriki kila mwaka karamu ya Pasaka, ambapo wote walikunywa divai mara nne, safari ya mwisho alikamilisha miujiza yake kwa kuigeuza iwe damu yake. “‘Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu’. Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, ‘Twaeni hiki, mgawanywe ninyi kwa ninyi; maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja’. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, ‘Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu’. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula, akisema, ‘Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu’” (Lk 22:15-20). “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je, si ushirika wa damu ya Kristo?” (1Kor 10:16).
Ushuhuda wa Biblia
Picha hapa
Agano Jipya linasimulia mara nne matendo na maneno ya Yesu ambayo alianzisha ibada hiyo na kuwakabidhi Mitume wake.
Simulizi la zamani zaidi ni lile la 1Kor 11:23-25. Likafuata lile la Mk 14:22-24; halafu yale ya Math 26:26-28 na Lk 22:19-20.
Kadiri ya ushuhuda huo, Yesu, katika karamu ya mwisho aliwagawia mitume wake mkate na divai akisema ndio mwili wake na damu yake vitakavyotolewa kama kafara kwa ondoleo la dhambi za umati, akawaagaiza wafanye vilevile kwa ukumbusho wake.
Hivyo Kanisa tangu hapo, linaendeleza ibada hiyo maalumu na ya msingi katika mazingira mbalimbali.
Simulizi la Paulo linafanana na lile la Mwinjili Luka na kufuata jinsi ekaristi ilivyoadhimishwa kati ya Wakristo wa mataifa; kumbe Mwinjili Marko na Mwinjili Mathayo waliripoti adhimisho lilivyokuwa kati ya Wakristo wa Kiyahudi.
Maendeleo
Mtakatifu Zosimas kutoa Ekaristi
katika Mtakatifu Maria wa Misri (hapa)
Ekaristi inaadhimishwa kwa mpangilio wa kupanda: waamini wanalishwa Neno la Mungu katika mimbari, halafu Mwili na Damu ya Kristo katika altare. Vilevile sehemu ya kwanza (liturujia ya Neno) inaleta masomo yakiwa na kilele katika Injili. Halafu katika sehemu ya pili (liturujia ya ekaristi) padri anafuata alichofanya Yesu katika karamu ya mwisho: anatwaa mkate na divai (kuandaa dhabihu zetu), anashukuru juu yake (sala kuu ya ekaristi inayogeuza dhabihu) na kuwapa waamini (komunyo, kilele cha yote, inayotugeuza ndani ya Kristo). Yesu mfufuka “aliwaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe... Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua” (Lk 24:27,30-31). “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali” (Mdo 2:42). “Siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu... akamega mkate, akala” (Mdo 20:7,11). Tusipofuata vizuri hatua za awali, hatutafaidika kweli na sakramenti: ndiyo sababu ni muhimu tuwahi ibada.
Kati ya namna mbalimbali za kuiadhimishwa, yalijitokeza mapokeo ya mashariki na ya magharibi. Kwa jumla mapokeo ya mashariki yanahusisha milango ya fahamu na ni ya fahari kuliko yale ya magharibi.
Ekaristi katika Kenya, Turkana kabila (hapa)
Teolojia
Ekaristi inahusiana sana na Pasaka, na kifo na ufufuko wa Yesu vilivyotokea kwenye sikukuu hiyo ya Wayahudi.
Kadiri ya Injili Yesu Kristo aliweka ekaristi wakati wa kuadhimisha karamu ya Pasaka ya Kiyahudi, akaipatia maana mpya kuhusiana na kifo na ufufuko wake.
Wakristo Orthodox wanaamini kwamba katika karamu ya Bwana wanakula na kunywa Mwili wa Damu ya Kristo. Katika sala kuu ya ekaristi padri anaporudia maneno ya Yesu juu ya mkate na divai, Roho Mtakatifu anavigeuza kwa dhati: mkate si tena mkate, wala divai si tena divai, ingawa maumbo yanabaki yaleyale kwa hisi zetu. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli” (Yoh 6:54-55). “Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana” (1Kor 11:27).
Baada ya mageuzo Yesu anabaki katika ekaristi moja kwa moja. Maumbo ya mkate na divai yanazidi kudokeza uwepo wake kama chakula na kinywaji chetu, hata kwa faida ya wagonjwa na wengineo wasiohudhuria. Ndiyo sababu tunazidi kumuabudu katika ekaristi, ingawa hatumuoni. “Tomaso alijibu, akamwambia, ‘Bwana wangu na Mungu wangu!’ Yesu akamwambia, ‘Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki” (Yoh 20:28-29).
Liturujia takatifu nchini Rwanda,
maandalizi kwa ajili ya Ekaristi (hapa)
Ekaristi ni kafara ambayo Yesu alimtolea Baba msalabani na anaendelea kumtolea kwa wokovu wetu. “Yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee... Kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima huyu naye awe na kitu cha kutoa” (Eb 7:24-25; 8:3). Katika ekaristi tunajiunga naye kwa kufanya ukumbusho wa kifo na ufufuko wake, tukimtolea tena Baba sadaka ya Mwili na Damu yake iliyolinganishwa na zile za Waisraeli na za Wapagani: “Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je, hawana shirika na madhabahu? Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani” (1Kor 10:18-21).
Ekaristi inaitwa sakramenti ya upendo kwa sababu kila unapofanyika ukumbusho wa sadaka hiyo pekee waamini wanazidi kujifunza na kupokea upendo ambao siku hiyo Yesu “ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo” (Yoh 13:1). Hivyo tunawezeshwa kutekeleza amri mpya aliyotuachia pamoja na ekaristi. “Amri mpya nawapa: Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo” (Yoh 13:34). Ni sharti tujitoe kama Yesu, tukijiunga na sadaka yake katika ibada na katika maisha. “Katika hili tumelifahamu pendo: kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma yake, je, upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli” (1Yoh 3:16-18).
Sakramenti inayokamilisha ubatizo na kipaimara ni ekaristi, iliyo kuu kuliko sakramenti zote kwa sababu ndiyo Yesu mzima, Mungu-mtu, katika maumbo ya mkate na divai. Walioshiriki kifumbo kifo na ufufuko wake wakapokea kwake paji la Roho Mtakatifu, wanaalikwa kukaribia mara kwa mara meza anapowalisha na kuwanywesha Mwili na Damu yake ili washiriki uhai wake kwa dhati zaidi na zaidi. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi” (Yoh 6:56-57). Ubatizo na kipaimara havirudiwi, vinadumu ndani ya mtu kama mifupa ambayo ekaristi ya mara kwa mara inazidi kuitia mwili na damu.
Kitubio au Upatanisho (hapa)
Kwa sababu hiyo, pamoja na Mpako wa wagonjwa ni kati ya sakramenti mbili za "uponyaji", zinazolenga afya ya roho na mwili inayoharibiwa na dhambi na ugonjwa.
Msingi wa teolojia yake katika Biblia
Kadiri ya imani hiyo, tunaweza kuona ina msingi gani katika ufunuo, hasa Agano Jipya. Ufafanuzi wake wa kichungaji unaweza kuwa kama ifuatavyo.
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa njia ya Mwanae. Yesu mfufuka aliwaonyesha Mitume alama ya mateso mwilini mwake, “akawavuvia, akawaambia, ‘Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23). Katika Kanisa tunafurahi kupewa msamaha wa dhambi kila tunapohitaji, mradi tutubu. Kwa njia ya mwandamizi wa Mitume, Yesu anatuambia, “Umesamehewa dhambi zako... Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani” (Lk 7:48,50). Si dhana wala hisia tu, bali ni neno la hakika tunalolipokea kwa masikio yetu.
Picha hapa |
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi zote, kwa sababu upendo mtiifu wa Mwanae aliyejitoa kuwa sadaka ya wokovu wetu unampendeza kuliko dhambi zote zinavyomchukiza. Ila hatuwezi kusamehewa dhambi ya kukataa neema ambayo Roho Mtakatifu anatusukuma tuamini na kutubu, kwa sababu pasipo imani na toba hapana msamaha. “Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa” (Math 12:31). “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure” (2Kor 6:1).
Mungu aliwapa watu amri ya kusamehe dhambi kwa sababu amependa washiriki katika kazi zake. Ametuumba kwa njia ya wazazi na kutulea na kutusaidia kwa njia ya wengine pia. Hasa ametuokoa kwa njia ya Yesu, ambaye yupo nasi sikuzote katika Mwili wake, yaani Kanisa, na katika wale walioshirikishwa mamlaka ya Mitume. “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:18-20).
Hivyo, tumuendee padri ili kuondolewa dhambi tulizotenda baada ya ubatizo, kwa kuwa hatuwezi kupokea msamaha tukikataa masharti yake, na Mungu ametupangia watu ambao watuondolee kwa niaba yake. “Watu wote na watoza ushuru waliposikia hayo, waliikiri haki ya Mungu, kwa kuwa wamebatizwa kwa ubatizo wa Yohane. Lakini, Mafarisayo na wanasheria walilipinga shauri la Mungu juu yao, kwa kuwa hawakubatizwa naye” (Lk 7:29-30). Yesu mwenyewe alikubali kubatizwa na Yohane ili atimize mpango wa Baba. “Yohane alitaka kumzuia, akisema, ‘Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu?’ Yesu akajibu akamwambia, ‘Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote” (Math 3:14-15). Je, sisi tukatae kumkimbilia padri wa Mungu ili kupokea huruma yake tunayoihitaji kuliko hewa?
Picha hapa
Tumuungamie padri dhambi zetu ili aweze kutushauri na kuamua kama tuko tayari kuondolewa. Tumweleze kwa unyofu makosa yote tuliyoyafanya na nia tuliyonayo ya kuyafidia na kutoyarudia. “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1:8-10). Tukumbuke tulivyo viungo vya Mwili mmoja, hivi kwamba dhambi zetu zimewadhuru wenzetu. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi na kuombeana, mpate kuponywa” (Yak 5:16). Kutokuwa tayari kufanya hivyo walau sirini kwa padri ni dalili ya kiburi na ya kutotubu.
Hata padri akiwa mkosefu, anaweza kutuondolea dhambi kwa niaba ya Mungu aliyempa mamlaka hiyo. Hatusamehewi na utakatifu wa padri, bali na huruma ya Baba kwa njia yake. Yeye anamtumia padri yeyote ili kuturahisishia kazi, tusihitaji kuchunguza kwanza ubora wa maisha yake, wala kwenda mbali tukampate mmoja asiye na dhambi. Tungefanyeje kuhakikisha ni mtakatifu, wakati hatuwezi kusoma moyo wake? Ingekuwa hivi, tusingepata kamwe hakika ya kusamehewa. Kumbe inatutosha kujua ni padri, kwamba Mungu amempa mamlaka ya kusamehe dhambi, kama Yesu alivyowapa Mitume siku tatu baada ya kumkimbia na hata kumkana. Kila padri anaweza kukiri, “Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa: ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi, ambao wa kwanza wao ni mimi” (1Tim 1:15). Amri ya kusamehe dhambi wamepewa watu, si malaika. “Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu” (2Kor 4:7).
Nje ya kitubio tunaweza kuondolewa dhambi tuliyotenda baada ya ubatizo, lakini ni vigumu zaidi, kwa sababu hatupati msaada wa sakramenti hiyo maalumu. Pamoja na nia ya kumuungamia padri mapema tunahitaji neema ya kutubu kikamilifu, si kwa kuhofia adhabu, bali kwa kumpenda Mungu tuliyemchukiza. “Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana” (Lk 7:47).
Tazama pia
Yesu Kristo - Mungu akawa mtu na mtu inakuwa kama mungu
Kanisa la Orthodox na Kanisa Katoliki
How Our Orthodox Brethren In Zambia Commune
Orthodoxy's Worship: The Sanctification of the Entire World
Historia ya Kanisa la Orthodox : Ukristo barani Afrika
A Liturgia Ortodoxa: "O Céu na Terra"
Δεν υπάρχουν σχόλια:
Δημοσίευση σχολίου