"...Licha ya kuwa nchi nyingi za bara la Afrika zina utajiri mkubwa wa maliasili kama vile almasi na dhahabu lakini ni asilimia 29 tu ya watu wa bara hilo ndio wanaonufaika na umeme na asilimia 65 kunufaika na mahitaji ya msingi maishani kama vile maji ya kunywa..."
Iran Swahili Radio

Wataalamu wanasema kutokea kwa ukame wa msimu katika baadhi
ya maeneo ya bara la Afrika kumepunguza sana mazao ya kilimo yakiwemo
mahindi katika maeneo hayo. Vilevile wanasema kupungua kwa malisho ya
mifugo kumesababisha upungufu wa bidhaa zinazotokana na wanyama hao
ikiwemo nyama na hivyo kuzidisha bei ya bidhaa hizo sokoni. Vilevile
kuzuka magonjwa ya kuambukiza na mapigano ya ndani katika baadhi ya nchi
za Kiafrika kumepelekea wafugaji na wakulima wengi kuyakimbia mashamba
yao na kutafuta usalama kwingineko.
Wajuzi wa mambo wanasema licha ya kuwa baadhi ya nchi za
Kiafrika kwa miaka mingi zimekuwa na mipango ya kutumia teknolojia ya
kisasa kwa shabaha ya kuimarisha mazao yao ya kilimo lakini mipango hiyo
haijatekelezwa kutokana na ughali wa mitambo na mashine za kuifanikisha
na pia hatua ya nchi tajiri za Magharibi ya kutotoa msaada wowote
katika uwanja huo.
Mbali na Zimbabwe na Ethiopia, Zambia, Botswana na Malawi
ni nchi nyingine za kusini mwa Afrika ambazo zinakabiliwa na tatizo la
upungufu mkubwa wa chakula. Mbali na nchi hizo migogoro ya kisiasa na
mapigano yanayoendelea huko Sudan Kusini, Somalia na nchi nyingine
nyingi za Kiafrika si tu kuwa ni mambo yanayohatarisha pakubwa usalama
wa chakula barani Afrika bali pia yanavuruga shughuli za masharika ya
kimataifa ya misaada za kuwafikia wahanga wa migogoro hiyo. Uhaba wa
umeme na maji na vilevile uchumi dhaifu ni mambo mengine yanayosemekana
kuchangia upungufu wa mazao katika sekta tofauti ikiwemo ya kilimo
barani Afrika. Licha ya kuwa nchi nyingi za bara la Afrika zina utajiri
mkubwa wa maliasili kama vile almasi na dhahabu lakini ni asilimia 29 tu
ya watu wa bara hilo ndio wanaonufaika na umeme na asilimia 65
kunufaika na mahitaji ya msingi maishani kama vile maji ya kunywa.
Wataalamu wanasema kuwa katika miongo michache inayokuja,
dunia kwa kuongezeka idadi ya watu itakabiliwa na changamoto kubwa za
maji na chakula. Hii ni katika hali ambayo bara la Afrika lina asilimia
60 ya ardhi za kilimo zisizotumika, ambapo kutumiwa vyema kwa ardhi hizo
kunaweza kuwa na mchango mkubwa na muhimu si tu katika kudhamini
usalama wa chakula wa bara hilo tu bali wa ulimwengu mzima kwa ujumla.
Kwa msingi huo ni wazi kuwa kumalizwa mivutano na mapigano
pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu ya bara la Afrika si tu ni jambo la
dharura katika jitihada za kulikomboa bara hilo kutokana na umasikini
wa chakula bali pia katika kupunguzwa umasikini katika upeo wa
kimataifa.
Δεν υπάρχουν σχόλια:
Δημοσίευση σχολίου