Σάββατο 17 Οκτωβρίου 2015

VIONGOZI KATIKA BARA LA AFRIKA
Kutoka AFRICAN BROTHERHOOD FOUNDATION

Kwenye kumbukumbu zangu hili neno uongozi sio suala geni hata kidogo. Kwa upande mwingine kila siku katika jamii zetu huwa tunasikia watu mbalimbali wanazungumzia yanayo husiana na uongozi kwa kutaja muhusika au wahusika wa uongozi ambao ni kiongozi au viongozi. Vilevile watu wanatafsiri neno uongozi kwa maelezo tofauti tofauti ili wapate maana.

Kona ya abfafrica inatafsiri na kuelezea maana ya uongozi; Uongozi ni dhana, taaluma inayompa muhusika madaraka, mamlaka na uwezo wa kuwawezesha wale anaowaongoza kuunganisha nguvu, ustadi na kuvitumia vipaji vyao ili kufikia malengo yao kama ni kiuchumi, kijamii ama kisiasa. Katika uongozi kuna aina ya uongozi, kama vile wakurithishana ambao mara nyingi ni utawala wa kifalme unaoendeshwa kwa njia ya urithi. Aina nyingine ni uongozi wa kuchaguliwa na watu ambao hutumia fursa ya kupiga kura kupitia chaguzi mbalimbali. Uongozi wa kimabavu daima yule mwenye mmlaka anaendesha utawala ule kwa mawazo yake bila ya kushirikisha watu anao waongoza bila ya kufuata misingi ya haki. Uongozi wa kuteuliwa na mamlaka za juu mfano raisi kumteua balozi, jaji, mkuu wa majeshi.

Kona ya abfafrica leo inapenda kuelezea juu ya uongozi wa Afrika ili kuipa jamii ya watu wa Afrika fursa ya kutambua viongozi wao waliowachagua na namna wanavyoendesha nchi zao. Uongozi bora ni ule unao simamia misingi ya utu, wenye kulenga maslahi ya watu, kutetea haki za binadamu, kuleta usawa bila ya kujali dini ama kabila la mtu. Pia viongozi wanapaswa kuwa watu wenye maadili mema yenye kulenga na kufuata taratibu na mwenendo wa kiafrika, kusimamia rasilimali za watu wanaowaongoza, kutetea watu wake na kuwapigania kwa nguvu moja, na kuwaunganisha watu wake na jamii zinazo wazunguka.

"Ni vizuri kuongoza ukiwa nyuma na kuwaweka wengine mbele, hasa mnapo sherehekea ushindi na wakati mambo mazuri yanapotokea. Na kukaa mstari wa mbele wakati kuna hatari. Kwa kufanya hivyo, watu watauheshimu uongozi wako.
Nelson Mandela." 


Swali linakuja, je, viongozi wa Afrika wanafanya haya?. Historia ya bara letu la Afrika inatuonesha namna viongozi waliopita walivyo kuwa na kiu kubwa ya kulifanya bara hili liwe moja ndio maana tarehe 25 mwezi 5 mwaka 1963 sahihi za viongozi 32 walioketi pale mjini Addis Ababa katika nchi ya Ethiopia, chini ya mwenyekiti wa kwanza hayati HAILLE SELASSIE 1, kiongozi mkuu wa Ethiopia wa wakati huo lengo ni kuinganisha Afrika katika masuala ya umoja na mshikamano wa nchi za Afrika na kuweza kuwa na sauti moja ya bara la afrika. Vilevile kuinua hali ya kimaisha ya waafrika waliotoka ndani mikono ya wakoloni, Vilevile walitaka kusaidia nchi zote zilizo kuwa bado hazijapata uhuru kuhakikisha zinakuwa huru. Mfano wa nchi hizi ni ZIMBABWE,AFRIKA YA KUSINI, ANGOLA nk. Ukitazama kwa undani viongozi wale kikubwa walichokitaka ni kufanya muungano wa kihistoria utakao lenga kupata Afrika moja.

"Mpaka itikadi inayolifanya tabaka fulani kuwa juu na jingine kuwa chini kuondolewa na kutokomezwa, kila sehemu itakua ni vita na mpaka pale ambapo hakutakua na raia wa daraja la kwanza na wale wa daraja la plili katika taifa lolote, mpaka rangi ya ngozi ya mtu haitakuwa na tija kuliko rangi ya macho yao. Na mpaka haki za binadamu zitakapo zingatiwa kwa wote bila kujali rangi, vita itakuwepo. Na mpaka ile siku ambayo, ndoto ya amani ya kudumu, uraia wa dunia, uongozi wa maadili ya kimataifa, itabakia kuwa ndoto ya kusadika inayohitajika kutimizwa na kamwe haijafikiwa, sasa kila sehemu ni vita" Haile Selasie 


1 Hata hivyo kona ya Abfafrica imebaini kuwa viongozi waliopita walifanya jitihada zao za dhati kwa ajili ya watu wao wa Afrika. Ukiangalia namna walivyo pambana na wakoloni nakuweza kuwatoa vilevile kwa kutuonesha njia ya muungano wa bara la Afrika. Leo hii viongozi walio wengi kati ya hawa tulionao wanashindwa kutimiza na kutekeleza majukumu yao kutokana wamekuwa vibaraka wa nchi za magharibi. Hii ni aibu kubwa! Hebu tazameni raia wenu wa bara hili wanavyopata tabu na kusumbuliwa huko ugaibuni! Hivi hii ndio Afrika ambayo JK Nyerere na Kwame Nkurumuah waliyo tuachia? Kumbukeni watu walijitoa sadaka kwa ajili ya bara hili. Daima tuwe tunakumbuka na kusoma historia ya nyuma. Na hivi vinavyo endelea sasa ni dhambi ya ubaguzi na unafiki tulizonazo miongoni mwetu. Tufikirieni kwa umakini wa hali ya juu kwa mitazamo chanya ili tuweze kupiga hatua. Hebu tazama hapa imefikia hatua baadhi ya vijana wa Afrika wanatamka maneno haya "Ni bora wangezaliwa mbwa Ulaya kuliko kuendelea kuishi afrika" hii sio lugha nzuri hata kidogo, ninaweza kusema ni ya kipuuzi. Lakini yote haya yanasababishwa na viongozi wetu wa Afrika kwa kushindwa kutekeleza sera zetu na kumthamini sana mtu wa nje ya bara hili. Chonde chonde viongozi wangu hebu acheni mara moja utumwa huo.

Afrika ina idadi ya watu wanakadiriwa kufika bilioni 1.033 kwa takwimu za mwaka 2013. Hebu viongozi wangu waleteni pamoja watu hawa ili tuzidi kuimarika kiuchumi. AFRICAN BROTHERHOOD FOUNDATION ina malengo ya kukutana na viongozi wote wa Afrika ili iwakumbushe na kuweza kujitathimini tulipotoka, tulipo na tunapokwenda. Inawezekana baadhi yao ulevi wa madaraka umewalevya na kushindwa kukumbuka yale yote yalio pita. Vilevile inawataka watu wasijinasibishe kwa nchi walizo toka tu, bali ni vyema zaidi kujivunia Afrika kwasababu wote asili yetu ni moja na haiwezi katu kupotea hii ni ngao yenye upeo wa harakati zetu zilipotokea hivyo hatuna budi kujivunia na kujitukuza kabla ya kutukuzwa kwa maana hiyo afrika ni moja bila ya shaka tunapaswa kujivunia afrika yetu.

Viongozi wote tunawaomba msiende makao makuu ya Afrika pale Ethiopia ilimradi muonekane mmeenda bali nendeni pale kwa lengo la kuutaka umoja wa Afrika una hakikisha maendeleo ya Afrika yanapatikana na maazimio yake yote yanatimizwa kwa wakati. Hii itatusaidia watu wote turudishe imani kwenu kama viongozi wetu kwasababu mtazuia wimbi kubwa la vijana lisikimbilie ugaibuni na nguvu kazi ya Afrika ikazidi kupungua. Hii italifanya bara hili kuweza kukua kiuchumi na kustawi zaidi katika ramani ya dunia.

Kuna baadhi ya viongozi wanatoka ugaibuni wanakuja Afrika kama ukiwasikiliza maneno yao, ni ya kuwakatisha tamaa waafrika wasiungane kwa sababu hilo ndio lengo lao kubwa kwa kuwa Afrika ikiungana hakuna tena gesi, mafuta, wala madini ya bure. Hivyo adui wao mkubwa ni muafrika anayejitambua na rafiki yao mkubwa ni muafrika muoga na mwenye kuzembea harakati za Afrika.

Kona ya Abfafrica inaona ajabu sana kuona baadhi ya viongozi wa afrika wanaona wanapendwa na wale viongozi wa magharibi kumbe wanatumiwa tu kama karatasi. Napenda kuwakumbusha wako wapi akina Savimbi wa Angola na Mabutu wa Zaire? Wakishakutumia watakumaliza tu! Ombi langu kwenu tuache mara moja kuwa vibaraka, tuitazame kwanza Afrika.

Bila ya kufanya hivyo kazi tulioachiwa na waasisi wa umoja wa Afrika, ambayo kazi kubwa ni kuhakisha Afrika inaungana na kuwa moja, maendeleo makubwa ya Afrika hayato patikana mpaka tuungane kwa ukweli. Matendo yanahitajika sana kuliko maneno. Mwendo mzima wa Afrika unapaswa uendeshwe na waafrika wenyewe. Tunamshukuru Mungu kwa kutujaalia rasilimali za kutosha vilevile kuweza kutupatia wataalamu wa fani mbalimbali hivyo basi ni jukumu kubwa la viongozi na uongozi wote wa Afrika kwa ujumla wake kuwatumia na kuwaleta pamoja watu wake.

Mungu ibariki Afrika. One Blood, One Love, One Africa, Forever!.

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου