Παρασκευή 16 Οκτωβρίου 2015

Kumalizika safari ya Rais Obama barani Afrika


Iran Swahili Radio, 29 Julai 2015

Kumalizika safari ya Rais Obama barani AfrikaRais Barack Obama wa Marekani jana baada ya adhuhuri aliondoka Addis Ababa Ethiopia na kuelekea Washington na kwa utaratibu kuhitimisha safari yake ya siku tano barani Afrika ambapo alizitembelea Kenya na Ethiopia. Akihutubu katika makao makuu ya Umoja wa Afrika, Rais Obama alizungumzia uhusiano wenye uwiano na bara la Afrika, vita dhidi ya ugaidi na demokrasia. Wakati Rais Obama alipoingia madarakani wananchi wengi wa Afrika hususan watu wake wa karibu nchini Kenya walifurahi sana. Walikuwa na matarajio makubwa na Rais huyo mwenye damu ya Afrika, hata hivyo sera za Marekani barani Afrika ziliendelea kama zilivyokuwa huko nyuma na hazikuwa na natija chanya na ya kuridhisha kama vile amani kwa bara hilo.
Fauka ya hayo hatua ya Marekani ya kuingilia mambo ya nchi nyingine iliandaa uwanja wa kutokea mivutano na migogoro kwa makumi ya nchi za Kiafrika na hali hiyo kupelekea kutokea vita kadhaa barani Afrika. Hatua za Marekani katika miaka ya hivi karibuni barani Afrika zinaonesha kuwa, serikali ya Washington mbali na kushindana kiuchumi na washindani wenzake kama China barani Afrika, ilichukua hatua ya kupanua harakati zake za kijeshi katika bara hilo. Kuasisiwa kikosi cha Marekani barani Afrika AFRICOM mwaka 2008 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi ni jambo linalotathminiwa katika uwanja huo. Katika hali ambayo kabla ya hapo vita vya siri vya Marekani nchini Somalia, Yemen, Libya na Mali vilikuwa vimefichuliwa, hivi sasa viongozi wa Marekani wametangaza wazi mpango wao wa kutuma wanajeshi wa nchi hiyo kwa uchache katika nchi 35 za Kiafrika. 
Jenerali Raymond Odierno Mkuu wa Vikosi vya Marekani amesisitiza katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Washington Times kwamba, kutumwa vikosi vya Marekani kunafanyika katika fremu ya stratejia ya nchi hiyo ya kutuma vikosi katika maeneo mbalimbali ya dunia ili ikilazimu iweze kuwa na radiamali ya haraka ya kukabiliana na changamoto itakayojitokeza. Ukweli wa mambo ni kuwa, viongozi wa Marekani wanaamini kuwa, bara la Afrika limo katika hali ya kubadilika na kuwa la kiistratejia katika uga wa kimataifa ambapo kuanzishwa vituo vya kijeshi barani humo ni miongoni mwa malengo ya Washington ya kuwa na satuwa na udhibiti barani humo. Kwa sasa kuna mamia ya wanajeshi wa Marekani nchini Niger. Nchini Chad pia kuna vikosi vya Marekani ambavyo vimetumwa huko kwa kisingizio cha ushirikiano wa kiusalama. 
Nchi ya Somalia nayo ni moja ya walengwa wakuu wa operesheni za kijeshi za Marekani yakiwemo mashambulio ya ndege zisizo na rubani. Serikali ya Obama pia  ilituma vikosi vya Marekani katika nchi kadhaa za katikati na mashariki mwa Afrika mwaka 2011 kwa kisingizio cha kufanya juhudi za kuwatia mbaroni viongozi wa kundi la waasi wa LRA wa kaskazini mwa Uganda. 
Vyombo vya Marekani vimesema kuwa, Washington inataka kuanzisha kituo cha kijeshi cha ndege zisizo na rubani nchini Niger au Burkina Faso ili kupitia kituo hicho iweze kuongoza operesheni za kijasusi kaskazini mwa Afrika. Kambi ya kijeshi ya Lemonnier ya Marekani nchini Djibouti nayo imo katika hali ya kupanuliwa na idadi ya wanajeshi wa Kimarekani walioko katika kambi hiyo wameongezeka. Hapana shaka kuwa, madai ya Marekani ya kupambana na ugaidi yangali yanatumiwa kama wenzo wa Washington wa kupanua hatua zake za kijeshi barani Afrika.

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου