Παρασκευή 16 Οκτωβρίου 2015

AFRIKA NA JINAMIZI LA UBINAFSI


African Brotherhood Foundation

Ni miaka mingi sasa toka wazee wetu,wanaharakati na wanamajumui kama Mwl J.K.Nyerere, Patrice Lumumba, Kwame Nkrumah, Booker T. Washington, Marcus Garvey na William du Bois watangulie mbele za haki. Ni ukweli usiopingika kwamba kimwili hatunao tena lakini kiroho na kifikra daima wapo pamoja nasi. Hawa wote walikuwa wazalendo na wapiganiaji haki za mtu mweusi. Siku zote walitamani kuona utu wa mtu mweusi unapatikana. Wanamajumui hawa hawakua tayari kuona mtu mweusi ananyanyaswa na kuonewa. Siku zote walipigania umoja baina ya waafrika na watu weusi kiujumla na sio maendeleo yao ili wapate utukufu binafsi( self glory). Hakika wazee wetu hawa Afrika kwao ilikua ni mwanzo na mwisho (Alfa na omega). Wanaharakati hawa kwao ilikua afrika kwanza Mimi badae...

"Gharama ya kutafuta uhuru ni bora kuliko malipo ya ukandamizaji".

Leo hii ni miaka kadhaa tangu wanamajui hawa watangulie mbele za haki. Swali la kujiuliza ni je, viongozi wa Afrika na waafrika kiujumla wanawaenzi vipi wazee hawa? Bila shaka wazee hawa hawaenziwi tena. Falsafa za wazee hawa zimetelekezwa. Waafrika kwa bahati mbaya au kwa makusudi kabisa wamepuuza falsafa na misingi ya wazee hawa. Wazee hawa wamezikwa na misingi yao ya uzalendo, umoja,mshikamano,upendo na amani baina ya waafrika.

Ndugu zangu, wakati wazee wetu kama kina Nyerere, Lumumba, Mandela, na Nkrumah wakiamini Afrika kwanza mimi baadae, viongozi wa sasa na waafrika walio wengi wametawaliwa na mimi kwanza nchi yangu baadae na sio Afrika tena. Asilimia kubwa ya waafrika ni wabinafsi au kwa lugha nyingine waswahili wanasema "wamimi". Wengi wanajali maslai binafsi na sio maslai ya waafrika kiujumla.

"Toka siku nyingi nia ya uovu mkubwa uliopandikizwa kwetu na wakoloni wanao ondoka, na ambao tunajipandikiza wenyewe katika hali yetu ya sasa ya utengano, ilikua ni kutuacha tumegawanyika katika mataifa yasiyojiweza kiuchumi ambayo hayathubutu kupiga hatua katika maendeleo ya ukweli.............".
Viongozi wa Afrika hawana uchungu na bara la Afrika. Uzalendo umebaki kwenye majukwaa ya kisiasa. Uzalendo kwa viongozi waafrika na waafrika kiujumla sio tena kitu cha kujivunia. Ukosefu wa uzalendo kwa waafrika kumepelekea kuongezeka kwa rushwa Afrika, njaa, vita za wenyewe kwa wenyewe, elimu duni, magonjwa na umasikini ulio kithiri. Inasikitisha sana kuona bara la pili kwa idadi kubwa ya watu, bara la pili kwa ukubwa na bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali duniani linaendelea kuwa tegemezi na maskini.

Ubinafsi kwa viongozi umepelekea wasaini mikataba mibovu yenye kuwanufaisha wao wenyewe, wajilimbikishie mali na wengine kuthubutu hata kuhamishia fedha zao kwenye akaunti za siri huko ughaibuni. Wakati viongozi wakifanya haya watoto wa shule wanakaa chini (sakafuni), shule hazina vitabu vya kutosha wala maabara. Wakati vijana wafrika wanashindwa kuendelea na masomo kwa kukosa mikopo ya vyuo vikuu, viongozi wa Afrika wameendelea kuona fahari kusafiri kwenda nchi za ulaya wakijua ndio fursa pekee ya kupiga picha na kushikana mikono na maraisi na mawaziri wakuu wa nchi kubwa zinazojiita zimeendelea.

Kwa upande mwingine waafrika ambao sio viongozi lakini wanao uwezo kifedha nao wanasakamwa na jinamizi la ubinafsi. Inasikitisha kuona matajiri wa Afrika wanatumia fedha nyingi kufadhili vyama vya siasa na wanasiasa lakini wengine wakithubutu kuwaruhusu mashabiki wa mpira wa miguu waingie bure katika viwanja kisha gharama zote atalipa yeye, lakini waafrika wangapi pale Amana hospitali wanachangia kitanda? Watoto wa shule wangapi Afrika wanakaa chini kwasababu ya ukosefu wa madawati? Kwanini hizo fedha wasiwasaidie waafrika hawa? Au kwasababu waafrika hawa wa kawaida hawana uwezo wa kutoa misamaha ya kodi kwa makampuni yao? Matajiri wakubwa wa Afrika lazima muache ubinafsi, vinginevyo Afrika itaendelea kuwaita maskini.

Inasikitisha sana kuona baadhi ya waafrika wapo tayari kutoa fedha nyingi kuwatunza waimbaji na wanenguaji wa bendi za muziki bila kujiuliza mara mbilimbili ili mradi tu wanamziki hawa wawaite "pedezyee fulani". Wakati mapedezyee hawa wakifanya hivyo,kuna waafrika Somalia wanakufa kwa njaa, vijiji kule Botswana havipitiki kwa ubovu wa barabara,waafrika katika hospitali ya Muhimbili Tanzania wanakufa kwa kukosa matibabu. Je,wanasubiri waafrika hawa waite "pedezye..." Kama wafanyavyo wanamuziki ndio wapeleke vitanda kule hospitali ya Peramiho Songea? Au madawati kule shule ya msingi Katubuka Kigoma? Waafrika mnaojiita mapedezye lazima mbadilike lasivyo Afrika itaendelea kutegemea mataifa ya kibepari wakati sisi wenyewe tukiamua tunaweza kuliendeleza bara letu.

Mwisho ningependa kutoa wito kwa waafrika wote waige mfano wa Booker T Washington aliyeamua kujitolea kujenga shule takribani 500, 'railway' kule Virginia na kuanzisha miradi mbalimbali kwajili ya kumkomboa mtu mweusi kule Marekani pasipo kuingojea serikali. Hivyo waafrika wote tuchukue jukumu la kuliendeleza bara letu bila kujali tofauti zetu za kidini, kikabila,kisiasa na kitaifa na sio kuziachia serikali peke yao.

"Afrika kwanza Mimi badae...."

One blood, one love, one Africa forever...

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου