Τετάρτη 14 Οκτωβρίου 2015

Historia ya Kanisa la Orthodox : Ukristo barani Afrika


 

Wakristo Orthodox Watakatifu wa Afrika (picha hapa)

Sw.wikipedia

Ukristo barani Afrika una historia ndefu inayokaribia miaka elfu mbili.
Ukristo uko Afrika katika wingi wa madhehebu yaliyopatikana katika historia ya Kanisa, baadhi katika bara hilo, baadhi katika mabara mengine.
Kwa sasa ndiyo dini kubwa zaidi barani, hasa Kusini kwa Sahara, pamoja na Uislamu ambao unaongoza Kaskazini kwa jangwa hilo.

Ustawi wa Ukristo leo

Leo karibu nusu ya Waafrika wote ni Wakristo. Lakini asilimia ya Wakristo inaweza kuwa ndogo katika nchi kadhaa na kubwa katika nchi nyingine. Katika Afrika Kaskazini Wakristo ni wachache. Kumbe ni wengi kwa theluthi mbili za bara kusini kwa Sahara.

Kwa jumla Wakristo wanaishi kati ya wafuasi wa dini nyingine, hasa Uislamu na dini za jadi.

Idadi yao inaongezeka haraka sana. Kila baada ya nukta nne Mwafrika mmoja anaingia Ukristo. Wengine huzaliwa katika familia ikiwa mzazi mmoja au wote wawili ni Wakristo tayari. Katika madhehebu mengi iko desturi ya kuwabatiza watoto wadogo. Ubatizo huo unawafanya kuwa wanakanisa. Wakikua watafundishwa na pengine kukaribishwa kwenye Kipaimara. Katika ibada hiyo kijana atarudia ahadi ya ubatizo wake na kuwekewa mikono na askofu au mchungaji mwingine na kuombewa ili Roho Mtakatifu amsaidie katika maisha yake ya Kikristo. Madhehebu mengine hayabatizi watoto wadogo. Yanaweza kuwapokea katika Kanisa kwa ibada maalumu lakini yanasubiri mpaka mtoto atakapokuwa mtu mzima, halafu apokee ubatizo na kuwa Mkristo rasmi.

Njia nyingine ya kukua kwa Kanisa ni kuongoka. Maana yake mtu asiye Mkristo anasikia habari za imani na kuvutiwa moyoni. Halafu anafika kwa kiongozi wa Kanisa na kupata mafundisho juu ya imani na maisha ya Kikristo. Halafu anaweza kubatizwa. Atakuwa mwanakanisa katika dhehebu fulani lakini ni vilevile Mkristo katika Kanisa moja takatifu la Bwana Yesu lililopo popote duniani. Wakristo Waafrika wengi kidogo ni watu walioongoka: waliwahi kuwa wafuasi wa dini nyingine (hasa dini za jadi, lakini wengine Uislamu), wakasikia Habari Njema wakaamua kumfuata Yesu. 


 Wakristo Orthodox wa Mwanza (picha hapa)
Historia

Wakati mwingine tunaweza kusikia kuwa Ukristo uliingizwa Afrika juzijuzi tu, na asili yake ni Ulaya. Hili si kweli. Ukristo ni imani ya kale sana katika Afrika. Tangu mwanzo wa Kanisa walikuwepo Wakristo Waafrika.

Ila Afrika Mashariki historia ya Ukristo si ndefu. Mwaka 1900 katika eneo la Tanzania ya leo Wakristo walikuwa elfu kadhaa tu. Ongezeko lilikuja haraka sana. Leo hii wako zaidi ya milioni 20. Wakati ule kati ya Watanganyika 100, Wakristo walikuwa 2 tu. Leo zaidi ya 50 kati ya Watanzania 100 ni Wakristo. 


Afrika na sehemu nyingine za dunia wakati wa Yesu

Miaka 2000 iliyopita mawasiliano kati ya nchi na nchi hayakuwa rahisi. Hapakuwa na redio wala simu wala ndege wala magari. Usafiri ulikuwa kwa miguu au kwa kupanda wanyama (k.v. farasi, ngamia, punda), halafu kwa meli za tanga. Meli hizo ziliweza kufuata pwani tu, hazikuwa imara kutosha kuvuka bahari kubwa.

Lakini hata kwa vyombo hivyo iliwezekana kufanya biashara kati ya Mediteranea na nchi za mbali kama Bara Hindi au Afrika Mashariki. Tunafahamu kitabu ambacho kiliandikwa mwaka 100 BK na kueleza usafiri wa baharini kutoka Misri hadi pwani ya Afrika Mashariki (iliyoitwa na Wagiriki "Azania"). Lakini watu waliojua habari hizo walikuwa wachache.

Jangwa la Sahara lilikuwa kizuizi kikuu cha mawasiliano na usafiri kati ya sehemu kubwa ya Afrika na sehemu nyingine. Mabara ya Amerika na Australia hayakujulikana na wataalamu wa Asia, Afrika na Ulaya.

Watu wengi waliamini dunia kuwa tambarare yenye umbo la duara (kama sahani), ingawa wataalamu wengine katika Misri walikwishagundua kwa njia ya kupima dunia kuwa ina umbo la chungwa. Lakini si watu wengi walioamini au kujali elimu hizo. Ilikuwa nje ya upeo wao. Hali hii ilibadilika tu karne nyingi baadaye, wakati meli za kuvuka hata bahari kubwa zilipopatikana.

Tukiona ya kwamba asili ya Ukristo ni eneo la Yerusalemu tunaweza kuelewa jinsi gani mitume wa Yesu waliweza kutumia usafiri uliopatikana wakati ule na kufika nchi zilizojulikana katika mazingira yao lakini hawakufika mbali zaidi.

Wakati wa Yesu Afrika Kaskazini pia ilikuwa chini ya utawala wa Roma. Wakati ule wakazi wake hawakuwa Waarabu. Kiutamaduni palikuwa na sehemu mbili: Misri upande wa Mashariki na nchi za Waberberi upande wa Magharibi. Nchi hizo za Waberberi (Moroko, Algeria, Tunisia na Libia za leo) zilikuwa pia na miji mingi walipokaa wahamiaji kutoka Italia waliotumia lugha ya Kilatini. Mji mkuu wa sehemu ile ni Karthago (karibu na Tunisi ya leo). Mji mwingine unaoonekana katika Biblia ni Kurene (kule Libia).

Misri ilikuwa kitovu cha elimu ya juu tangu karne nyingi. Mji mkuu wa Misri ulikuwa Aleksandria. Eneo la utawala wa Roma lilifika mpakani mwa Sudani ya leo (eneo lililoitwa "Nubia").

Nchi hizo hazikuwa na mawasiliano mengi na nchi za kusini mwa jangwa la Sahara lililozuia usafiri. Hivyo imani ya Kikristo ilifika haraka katika sehemu ya Kaskazini kwa Sahara ila haikuvuka jangwa hilo kubwa. Lakini mawasiliano yalikuwepo na sehemu za Ulaya Kusini na Asia, hasa kupitia Bahari ya Kati. Ilikuwa rahisi kwa mitume wa Kristo kutumia mawasiliano hayo yaliyokuwepo tayari.

Watu wa Mediteraneo walifanya tayari biashara kwa meli na pwani ya Afrika Mashariki. Tunaweza kuwaza ya kwamba wafanyabiashara Wakristo walitembelea mapema sehemu hizo pia lakini hakuna kumbukumbu yoyote kama walihubiri n.k.

Nchi hizo za Afrika Kaskazini zilikuwa tajiri. Hali ya hewa wakati ule ilikuwa afadhali kwa kilimo kuliko leo. Milima ya Atlas ilijaa misitu. Katika Algeria na Tunisia ya leo ililimwa ngano kwa wingi na kuilisha Italia. Hata jina la "Afrika" lina asili yake katika kipindi cha Kiroma. "Afrika" ilikuwa jina la mkoa mmoja uitwao leo Tunisia. Kutoka kule jina hilo lilitumika baadaye kwa sehemu nyingine za bara hilo.

Kwa jumla watu walifuata dini zao za asili za kuabudu miungu mingi. Palikuwa na mchanganyiko wa imani mbalimbali. Wanajeshi Waroma waliokaa katika nchi nyingi walileta miungu yao na kuwajengea mahekalu pale walipokaa. Kule Misri na sehemu za Kurene waliishi pia Wayahudi wengi waliotumia hasa lugha ya Kigiriki. Kwa njia ya Wayahudi hao habari za Mungu mmoja zilikuwa zinasikika sehemu nyingi. 


"Filipo mwinjilisti alikutana na msafiri kutoka Kushi akambatiza..." (picha hapa)

Watu wa Afrika Kaskazini walisafiri na kukaa pia katika miji ya Ulaya na Asia. Kutokana na mawasiliano mazuri tunaona Waafrika mbalimbali katika taarifa za Agano Jipya. Tuone mifano: - Yesu alipobeba msalaba wake kule Yerusalemu akaanguka chini. Maaskari wakamkamata mtu aliyepita mtaani jina lake ni Simoni wa Kurene. Jina linaonyesha ya kwamba alikuwa mgeni kutoka Kurene (Libia). (Lk 23:26) - wakati wa ushirika wa kwanza kule Yerusalemu, Filipo mwinjilisti alikutana na msafiri kutoka Kushi akambatiza. Kushi ni jina la kale la sehemu ya Sudan Kusini ya leo (matoleo mengine ya Biblia hutafsiri: Mhabeshi au Mwethopia). (Mdo 8:26 n.k.). - katika ushirika wa mji mkubwa wa Antiokia (Asia Magharibi) tunasikia juu ya watu wa asili ya Afrika waliokuwa viongozi wa ushirika huo. Mmoja ni Lukio Mkurene. Mwingine ni "Simeoni aitwaye Nigeri". Neno "Nigeri" linatafsiriwa "Mweusi". Kumbe hata huyu anaonekana ametokea Afrika kutokana na rangi yake. (Mdo 13)

Haya yote si ajabu. Nchi za Misri mpaka Sudan na Afrika Kaskazini-Magharibi zilikuwa sehemu ya Dola la Roma wakati Ukristo ulipoanza kuenea.

Yesu mwenyewe alikaa miaka kadhaa Afrika. Alitoka nje ya Israeli-Palestina mara moja tu katika utoto wake wakati wazazi wake walipokimbilia pamoja naye Misri kwa sababu Mfalme Herode Mkuu alitaka kumwua mtoto Yesu. Mpaka leo Wakristo wenyeji wa Misri wanatunza kumbukumbu ya Familia Takatifu katika nchi yao. Makanisa mbalimbali yapo mahali panapokumbukwa ya kwamba Yosefu, Bikira Maria na mtoto Yesu walipumzika. 


Asili ya Ukristo nchini Misri


Picha hapa
 
Hatuna habari ndani ya Biblia juu ya shirika za kwanza zilizoundwa kule. Lakini Wakristo wa Misri wanamkumbuka Marko Mwinjili aliyefika Aleksandria na kuhubiri Habari Njema Afrika hata kuanzisha Kanisa pale Misri. Ndiye hasa mwinjilisti wa Afrika. Marko alikuwa amesafiri na Mtume Petro kama mwanafunzi wake.

Hakuwahi kuwa mwanafunzi wa Yesu, lakini aliandika Injili, yaani taarifa juu ya maisha na mafundisho yake. Alikuwa mwandishi wa kwanza wa habari hizo. Mtume Mathayo na Luka mwinjili walitumia taarifa ya Marko walipoandika Injili zao.

Anasemekana alikufa akiwa shahidi wa imani wakati wa mateso ya kwanza chini ya serikali ya Roma. Anakumbukwa kama Askofu wa kwanza wa Aleksandria. Ndiyo sababu mpaka leo Askofu Mkuu wa Aleksandria huitwa "Mwandamizi wa Marko". 


Ushujaa wakati wa dhuluma (64-309)

Tuna habari nyingi juu ya Wakristo kule Misri na Karthago (magofu yake yako nchini Tunisia) wakati wa karne ya 2. Habari hizo zinaeleza maisha na mateso yao.

Hao na Wakristo wa kwanza walio wengi waliishi chini ya serikali ya Roma. Kwa jumla hiyo iliwaruhusu watu wote kuendelea na desturi na dini zao. Serikali iliona ni muhimu kuabudu miungu yote kwani ingekuwa hatari mungu fulani angesahauliwa hata kusababisha akasirike.

Matendo ya Mitume 17:16-23 inasimulia kwamba Mtume Paulo alishangaa kuona sanamu nyingi za miungu kule Athene. Kati ya sanamu hizo aliona madhahabu (altare) yaliyotengwa kwa ajili ya "Mungu asiyejulikana". Kumbe serikali ya Athene iliogopa kumsahau mungu yeyote ikatoa sadaka za tahadhari.

Kaisari naye, yaani Mfalme Mkuu wa Roma, alipewa heshima ya kimungu. Raia walitakiwa kushiriki ibada za kumtolea sadaka mbele ya sanamu zake. Kwa watu wengi waliozoea kuabudu miungu mingi haikuwa vigumu sana kumwingiza Kaisari kama mungu wa nyongeza katika mawazo yao. Lakini kwa Wakristo haikuwezekana kushiriki ibada hizo. Kwa hiyo walionekana kama maadui wa serikali. Walikamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani.

Ukali wa mateso ulitegemea siasa ya wakuu wa mikoa ya Kiroma. Wakati mwingine waliweza kujipatia sifa wakitoa taarifa ya kwamba wamekamata Wakristo wengi na kuwahukumu. Wakati mwingine waliona afadhali kuwaacha Wakristo na kutosababisha vurugu katika mkoa. Nje ya suala la kidini Wakristo walikuwa raia wema. Perpetua na Felista

Mnamo mwaka 203 B.K. aliishi mama kijana mwenye miaka 22 kwa jina Perpetua katika mji mkubwa wa Karthago. Perpetua alitokea familia tajiri na kuwa na mtoto wa kiume. Wazazi wake walikuwa wanaheshimiwa sana.

Kumbe Perpetua akashtakiwa kuwa Mkristo akakamatwa. Baba akamwendea mkuu wa mkoa wakapatana Perpetua atoe sadaka mbele ya sanamu ya Kaisari ili shtaka lifutwe. Kutoa sadaka maana yake ilikuwa kushika nafaka kidogo na kuitupa kwenye karai ya mkaa uliowaka mbele ya sanamu. Baba akamweleza mtoto wake gerezani alivyopatana na mkuu wa mkoa. Perpetua akakataa. Baba akamsihi akamwomba asilete aibu juu ya wazazi wake na amhurumie mtoto wake mdogo. Perpetua akamjibu baba ya kuwa tendo hilo halipatani na imani yake.

Felista alikuwa msichana Mkristo na wanawake hao wawili walikuwa marafiki ingawa Felista alikuwa mtumwa. Akafungwa pamoja na Perpetua na vijana watatu. Walipokataa kutoa sadaka wakapewa wote adhabu ya kifo.

Hao vijana Wakristo watano wakapelekwa katika uwanja wa michezo wa Karthago. Watu wengi wakatazama. Kuua wakosaji kulikuwa kama mchezo au burudani kwa wakazi wa miji. Walizoea kutazama maonyesho ya kuua wakosaji wenye hukumu ya mauti. Vijana Wakristo waliposimama uwanjani milango ya chini ikafunguliwa. Wanyamapori wakali waliokuwa wanahifadhiwa katika vyumba vya chini katika uwanja huo, wakiwekwa tayari ili kuwararua Wakristo wakatokea. Kuwatupa Wakristo mbele ya wanyama wakali ilifanywa kama onyesho la kuburudisha halaiki. Hao vijana wakashambuliwa na wanyama; wengine wakawaua na wengine wakajeruhiwa vibaya. Mwishoni wote waliojeruhiwa waliuawa kwa upanga

 

Maonyesho hayo yalikusudiwa kutisha watu waogope kuwa Wakristo. Lakini yakageuka kampeni kwa ajili ya Ukristo, kwa sababu watazamaji walianza kujiuliza: Je, watu hao wana kosa gani? Ni imani gani inayowapa nguvu ya kusimama mbele ya wanyama mwitu na kuuawa badala ya kutoa sadaka mbele ya sanamu? Kwa nini wale wanaokufa hivyo wanajulikana kuwa watu wasioiba wala kusema uongo, lakini wengine wenye tabia mbaya hawana matatizo wakitoa sadaka tu mbele ya sanamu? Kumbe damu ya mashahidi ilikuwa mbegu ya kukua kwa Kanisa

Farakano la Donato

Wakati Roma ilipotawala Wakristo wengi Waafrika walionyesha uhodari kwa kutokana imani yao na kufa kama mashahidi wa Yesu. Mfano huo ulisababisha Wapagani wengi kuwa Wakristo. Lakini si wote walisimama imara mbele ya vitisho. Wengi wakatoa sadaka mbele ya sanamu wakatubu baadaye na kuomba wasamehewe udhaifu huo. Wengine waliwahonga maafisa wa serikali wakanunua vyeti vilivyothibitisha ya kwamba walitoa sadaka zile ingawa haikuwa kweli. Katika eneo la Karthago jambo hili lilisababisha farakano ndani ya Kanisa lililoitwa kwa jina la askofu Donato Mkuu


Wafiadini nchini Misri

Katika karne ya 3 mateso yalikuwa makali hasa kule Misri. Katika miji mikubwa kama Aleksandria watu wengi walikuwa Wakristo. Machoni pa wakuu wa serikali hali hiyo ilikuwa uasi. Wakaona ni lazima kuzima uasi huo.

Kati ya miaka 302 na 308 B.K. maelfu wakauawa kule Aleksandria. Wakakatwa vichwa na maaskari, wakapelekwa katika kiwanja cha michezo mbele ya wanyama mwitu, wakachomwa moto. Lakini idadi ya Wakristo waliokuwa tayari kufa ilizidi uwezo wa serikali wa kuwaua.

Kumbe mwaka 312 ilikuwa kama ukombozi kwa mji wa Aleksandria. Kaisari mpya, kwa jina Konstantino Mkuu akatangaza mwisho wa mateso. Akatoa sheria ya kuwa Ukristo ni dini halali katika Dola la Roma.
Urithi wa Misri kwa Kanisa zima: elimu na umonaki

Misri ilikuwa kitovu muhimu cha Ukristo wa kale. Uhodari wa Wakristo wake ulishinda dhuluma za serikali ya Kiroma. Katika mapambano hayo Wakristo Wamisri wakaunda silaha mbili ambazo zimekuwa muhimu katika Kanisa zima mpaka leo: 1. Elimu ya Kikristo 2. Utaratibu wa umonaki


Mt Cyprian ya Karthage, 258 B.K. (picha hapa)
 
Elimu ya kikristo: Chuo cha Aleksandria

Jiji la Aleksandria lilikuwa na maktaba kubwa kuliko zote duniani. Wakati ule haikujulikana jinsi ya kupiga chapa vitabu. Kila kitabu kiliandikwa kwa mkono kikawa na bei kubwa sana. Kununua kitabu kulikuwa na gharama zinazofanana na ile ya kununua gari leo. Kwa hiyo elimu ilikuwa na thamani kubwa, na maktaba kubwa ilikuwa na thamani kupita kiasi. Wataalamu toka pande zote za dunia walifika Aleksandria, mji wa elimu, ili kusoma na kunakili vitabu. Si ajabu kwamba Agano la Kale lote lilitafsiriwa kwa mara ya kwanza katika lugha ya Kigiriki huko Aleksandria mwaka 150 hivi K.K.

Hivyo Wakristo wa Aleksandria walijisikia hawana budi kuwa tayari kujadiliana na watu wenye elimu. Wawe tayari kujibu maswali yao juu ya Injili hata kutetea imani kwenye ngazi inayolingana na elimu ya hali ya juu. Wakristo wenye elimu walijitolea kuelimisha Wakristo wenzao. Katika mafundisho hayo kilitokea chuo cha Kikristo cha kwanza. Masomo yake yalihusu imani na Biblia lakini pia elimu kwa jumla. Falsafa ilikuwa muhimu katika mawazo ya wataalamu hata katika mafundisho ya kidini ya Wapagani na Wayahudi. Basi, ilionekana afadhali mwalimu Mkristo ajue falsafa na awe na msimamo wake juu ya uhusiano kati ya falsafa na imani ya Kikristo.

Chuo cha Aleksandria kilipata sifa chini ya Panteno. Mnamo mwaka 200 BK huyo aliacha uongozi wa chuo akawa mmisionari huko Bara Hindi. Aliyemfuata alikuwa Klementi wa Aleksandria aliyefaulu sana kuvuta Wapagani wenye elimu kumpokea Kristo. 


 
Klemens wa Aleksandria

Mwanafunzi wake mashuhuri alikuwa Origene, ambaye baadaye akapewa uongozi wa chuo hicho. Alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 25. Origene alikuwa mtaalamu wa pekee: ndiye wa kwanza kutumia njia ya kisayansi katika kuchunguza fasiri za Biblia. Pamoja na makarani wake akaandika maneno yote ya Kiebrania ya Biblia pamoja na fasiri zake katika nguzo sita kwenye ngozi kubwa. Njia hiyo ilisaidia kuona mara moja makosa au udhaifu katika fasiri hizo. Aliwafundisha vijana wengi kutumia akili yao katika kutafakari imani kwani akili ni kipawa cha Mungu.

Kwa njia hiyo Chuo cha Aleksandria kimekuwa mwanzo wa elimu ya juu katika Ukristo. Mpaka leo ni kawaida kwamba mtumishi wa Kanisa awe na elimu. Wachungaji, mapadri na watawa wanasomeshwa katika vyuo mbalimbali hadi ngazi ya chuo kikuu. Ukristo umekuwa imani ya wasomi. Asili ya jambo hilo ni katika juhudi za Wakristo wa Misri. 


Utawa na umonaki - maisha ya pekee 


Picha hapa
 
Watawa ni Wakristo walioamua kuishi kwa njia ya pekee. Mara nyingi tumezoea kuwaona katika Kanisa Katoliki (=Orthodox). Lakini wako vilevile kati ya Waanglikana na Walutheri, ingawa si wengi. Ulaya wako hata masista Wamoravian na Wabaptisti.

Mtawa amepokea katika maisha yake ushauri wa mtume Paulo (ambaye hakuoa): «Nawaambia wale wasiooa bado, Ni heri wakae kama nilivyo» 1Kor 7:8. Yesu mwenyewe aliwahi kueleza ya kwamba watakuwepo wale watakaochagua maisha ya pekee bila familia na uzazi kwa ajili ya Ufalme wa Mungu (Mt 19:12: "Wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni»).

Kwa jumla watawa ni kundi muhimu linalosaidia sana kazi ya kiroho katika Ukristo. Wako huru kuliko wengine kujitolea katika huduma za Kanisa, kwani hawalazimiki kufikiria maendeleo ya watoto wao. Watawa wanaweza kuishi peke yao lakini mara nyingi wanajiunga na shirika au jumuiya na kuweka nadhiri za useja mtakatifu, ufukara na utiifu.

Asili ya jumuiya hizo iko Misri. Katika karne ya 3 mateso yalizidi chini ya serikali ya Waroma Wapagani. Wakristo wengine walijificha jangwani wakiogopa kulazimishwa kutoa sadaka kwa sanamu. Wengine waliona jinsi familia yao ilivyouawa katika dhuluma za kidini. Wengine karibu walikata tamaa wakiona Wakristo wengine walivyokana imani kwa kuogopa mateso. Kumbe wengine hawakuona raha tena katika maisha ya kawaida, wakajitenga na dunia wakaenda porini kuishi kule maisha ya kufunga na kusali.

Watawa hao waliitwa kwa jina la Kigiriki "wamonaki" (monos= moja; monakos= anayekaa peke yake). Walikaa jangwani katika maeneo yaliyokuwa mbali na miji na vitovu vya utawala wa Kiroma. Lakini waliheshimiwa sana na wananchi wa kawaida. Walitumia muda mwingi wakisali na kusoma Biblia. Watu wakazoea kuwaendea kuomba ushauri wao katika mambo ya kiroho au maisha kwa ujumla, kuombewa katika magonjwa n.k. Wengine walizoea kupokea zawadi za wanavijiji wakaelekea maisha ya kuombaomba.

Wamonaki wa kwanza walikaa kila mmoja peke yake bila kushirikiana. Antoni wa Misri alikuwa mmojawao, naye akaona umuhimu wa kuweka utaratibu fulani kati ya wamonaki wenzake. 


 
Mt Pakomi na malaika (hapa)

Mwanafunzi wake Pakomi aliendeleza mkazo wake akawaunganisha wamonaki mahali pamoja akawapa utaratibu wa kazi na sala. Katika utaratibu huo kila mmonaki (pia masista katika mashirika yao) hutoa ahadi au nadhiri tatu: 1. Useja mtakatifu: atachagua maisha bila ndoa; badala yake kujiunga na shirika la wenzake kama familia ya kiroho. 2. Ufukara: ataacha mali yake ya binafsi na hatatafuta tena utajiri wa kidunia. 3. Utii: atamtii mkuu wa shirika hilo aliyechaguliwa kati yao (huitwa "Abba/Abati") na kutii taratibu za ushirika wake.

 
Mtakatifu Siglitiki, "mama ya jangwa"
 
Utaratibu huo wa umonaki ulienea haraka: watawa wakaanza kukaa na kufanya kazi pamoja ili kujipatia mahitaji yao wenyewe. Baadaye vituo vya wamonaki vilikuwa vitovu vya elimu ambapo sehemu ya wamonaki walisoma, kuandika (au kunakili) vitabu, kuanzisha shule n.k.

Leo hii mashirika ya watawa ni maelfu. Kwa kawaida kila shirika lina mkazo wake wa pekee, kama vile maisha ya kimya katika sala au huduma za upendo: hospitali, nyumba za mayatima, ufundishaji, uinjilishaji, misheni, au n.k. Hivyo mtawa anaweza kuwa na maisha ya kutotoka katika nyumba ya shirika lake au anaweza kuishi kati ya Wakristo na wasio Wakristo akiwatolea huduma zake. 


Wamisionari Wamisri katika mabara matatu

Panteno wa Chuo cha Aleksandria alikwenda India kuhubiri Injili. Wamisionari wa Kanisa la Misri walianzisha Kanisa katika Sudan, Sudan Kusini na Ethiopia za leo. Hata sehemu mbalimbali za Ulaya zinakumbuka wamisionari kutoka Afrika waliohubiri huko Injili wakati wa Dola la Roma. Askari Wamisri katika jeshi la Roma walikaa miaka mingi Uswisi na kwingineko. Kati yao kulikuwa na Wakristo waliohubiri huko Injili kwa mara ya kwanza. Mji wa Zurich mpaka leo hii unaonyesha katika nembo yake majina ya Wamisri watatu waliokuwa wainjilisti wa kwanza wa eneo lake. Kule Ireland Wamisri waliunda monasteri mnamo mwaka 500 na kufundisha Injili. Waireland wanafunzi wa Waafrika hao ndio wainjilisti wa Ujerumani na Uholanzi baadaye. 


Ukristo kuenea Sudan hadi Ethiopia


Mt Moshe kutoka Ethiopia (picha hapa)

Jangwa kubwa la Sahara lilifanya mawasiliano yote kati ya Afrika Kaskazini na sehemu zingine za bara kuwa magumu. Lakini tangu zamani mto Nile ulisaidia biashara na athari za kiutamaduni na za kisiasa kuvuka kanda la jangwa. Hivyo upo uhusiano wa pekee kati ya Misri na eneo linaloitwa leo "Sudan".

Zamani nchi hiyo kusini kwa Misri iliitwa kwa jumla "Nubia"; sehemu moja ilijulikana kwa miaka mingi kwa jina la "Kushi". Mdo 8 inaonyesha kwamba safari kati ya Kushi (Sudan) na Misri mpaka Yerusalemu zilikuwa kawaida. Njiani Filipo alimbatiza "towashi wa Kushi" yaani afisa wa serikali ya malkia Kandake wa Kushi katika mji mkuu wa Meroe (Agano Jipya tafsiri ya Kiswahili cha Kisasa linatumia hapa kwa kosa jina la "Ethiopia"). Lakini hatuna habari zaidi kama huyo afisa alihubiri Injili kwao.

Kuanzia karne ya 3 athari za Ukristo katika Nubia zinajulikana. Wamonaki Wamisri walihubiri Injili huko. Kuanzia mwaka 600 wakazi wengi wa Kushi walikuwa Wakristo. Makanisa mengi tena makubwa yalijengwa na kupambwa katika miji mikubwa kama Dongola na Soba. Kwa miaka elfu moja utamaduni wa Kikristo uliendelea. Kutoka Dongola wamisionari walifika kusini mwa Sahara mpaka eneo la Tibesti (yaani Chad ya leo) ambapo maghofu yanaonyesha alama za Ukristo kule.

Kusini-Mashariki kwa Kushi tunakuta eneo kubwa lenye milima mirefu inayosimama kama mnara katika tambarare ya nchi jirani. Ni nyanda za juu za Ethiopia au Uhabeshi. Mnamo mwaka 300 B.K. kulikuwa na ufalme katika eneo la Aksum (Ethiopia ya leo).

Wakati alipotawala Kaisari Konstantino kule Roma, meli moja ilikuwa safarini kutoka Shamu kwenda Bara Hindi ikaharibika kwenye pwani ya Ethiopia. Vijana wawili waliokolewa wakapelekwa mbele ya mfalme kule Aksum. Mmojawao kwa jina Frumensyo alipata haraka sifa za kuwa mwenye elimu na hekima. Akapanda ngazi kuwa mshauri wa mfalme na mwalimu wa mwana wa mfalme aliyeitwa Ezana. Frumensyo aliweza kupanda mbegu za imani moyoni mwa kijana huyo. Baada ya kuwa mfalme, Ezana akaendelea kumtumia Frumensyo kama mshauri wake. 


 
Picha hapa
 
Siku moja Frumensyo aliomba ruhusa ya mfalme aende nyumbani kuangalia kama wazazi wake bado wanaishi. Mfalme akamruhusu akamwomba atafute kule walimu wanaoweza kufundisha elimu aliyokuwa nayo Frumensyo pamoja na imani ya Kikristo. Frumensyo akamwendea Askofu Mkuu wa Misri aliyemweka wakfu kuwa askofu kwa ajili ya Waethiopia. Hivyo Kanisa lilianza katika nyanda za juu za Ethiopia. Mfalme Ezana akabatizwa akifuatwa na watu wengi wa makao makuu.

Baadaye kule Ethiopia walifika wamonaki kutoka Misri na Shamu. Ndio walioanza kufundisha na kuwabatiza Wahabeshi wengi. Ndio mwanzo wa taifa la Kikristo la Ethiopia. Wahabeshi wametunza urithi wao wa Kikristo mpaka leo. Ukristo wao unafuata mapokeo ya Waorthodoksi wa Mashariki yalivyo hata Misri. Mpaka karne ya 20 walipokea Maaskofu wao wote kutoka Kanisa la Kikopti la Misri


Mabadiliko katika karne ya 7: kuja kwa Uislamu

Labda tumeshangaa kusikia ya kwamba leo hii wako Wakristo milioni kadhaa kule Misri, kwa sababu tumesikia mara kwa mara ya kwamba wenyeji wa Misri ni Waarabu na Waislamu. Kumbe katika karne saba za kwanza baada ya Kristo hali ilikuwa tofauti. Afrika Kaskazini ilikuwa nchi ya Wakristo, lakini baadaye yalitokea mageuzi makubwa yaliyokuwa muhimu sana katika historia ya Afrika: uenezi wa Uislamu.

Mnamo mwaka 610 B.K. sehemu kubwa ya Afrika Kaskazini iliunganika tena chini ya Dola la Roma lililotawaliwa kutoka mji wa Bizanti (Roma ya mashariki). Lakini utawala huo ulikuwa hafifu kulingana na zamani za Roma ya Kale.

Wenyeji wa Misri na mkoa wa "Afrika" (= Tunisia ya leo) walipinga utawala wa Bizanti. Wakristo wengi katika nchi hizo walikataa usimamizi wa Askofu Mkuu wa Bizanti wakiwafuata viongozi wao wa kitaifa. Viongozi wa Kanisa la Kikopti (Misri) waliteswa na serikali ya Bizanti. Dola la Roma ya Mashariki ilichosha nguvu zake vitani dhidi ya majirani yao wa Uajemi na makabila yasiyostaarabika kutoka kaskazini.

Hali hii ilibadilika ghafla mwaka 640 B.K. Habari za imani mpya kati ya Waarabu zilisikika tangu mwaka 622 kutoka eneo la Maka na Madina. Kiongozi mpya aliyeitwa Muhamad aliunganisha makabila yote ya Waarabu katika jina la Mungu mmoja, "Allah".


 

Baada ya kifo cha Muhamad wafuasi wake walitoka nje ya jangwa la Uarabuni na kushambulia maeneo jirani ya Bizanti na Uajemi. Walipigana na majeshi ya nchi hizo na kuyashinda. Mwaka 640 waliingia Misri. Baadhi ya wenyeji Wakopti waliwapokea kwa matumaini ya kuwa watamaliza utawala wa Bizanti. Jeshi la Bizanti lilishindwa kwa kukosa msaada wa wazalendo. Kiongozi Mwislamu aliahidi madhehebu yote yataheshimiwa. Alifanya mkataba na Wakristo waendelee na ibada zao na desturi zao.

Lakini baada ya muda Wamisri waliona ya kwamba wamekuwa watu wa ngazi ya chini nchi mwao. Mabwana wapya walianza kubadilisha utamaduni wa nchi. Aliyejiunga na Uislamu na kujifunza Kiarabu alikubalika lakini Wakristo wenyeji waliotunza urithi wao walibaguliwa. Majaribio yote ya kupigania uhuru yaligandamizwa vikali.

Miaka mia iliyofuata Waislamu waliteka sehemu iliyobaki ya Afrika Kaskazini. Miaka 670/696 waliteka mkoa wa "Afrika" ya Kiroma pamoja na Karthago (Tunisia ya leo). Mwaka 711 wakavuka mlangobahari na kuingia Hispania (Ulaya Kusini). Walifika mpaka Ufaransa wakarudishwa na wenyeji mwaka 732 lakini walitawala sehemu za Hispania kwa karne saba zilizofuata.

Kule Tunisia na Algeria Ukristo ulikuwa dhaifu kutokana na mafarakano mengi ya miaka ya nyuma na dhuluma za Wavandali. Baada ya karne za kulaumiana kati ya Wakristo, wengine walikuwa na wasiwasi juu ya ukweli wa mafundisho ya Kanisa. Katika nchi za jirani (Italia na Hispania) vita vikali vilipigwa kati ya Waarabu walioshambulia na Wakristo waliojitetea. Labda hali hiyo iliongeza moyo wa Waislamu kutovumilia kuwepo kwa Wakristo. Kanisa katika Afrika Kaskazini lilipotea baada ya karne chache.
 


Sababu za Wakristo wengi kugeuka Waislamu

Wafuasi wa Muhammad walishambulia maeneo jirani ya Waroma wa Bizanti hasa Afrika Kaskazini. Uislamu ulienea haraka sana kwa nguvu ya kijeshi katika nchi zilizokuwa na Wakristo wengi.

Sababu kubwa ya udhaifu wa Wakristo Waorthodoksi ilikuwa mafarakano kati yao, na hasa majaribio ya serikali ya Bizanti kuwalazimisha Wakristo wote kufuata uongozi wake, wakiitumia na kuitawala dini kama nguzo ya siasa yake. Lakini mambo ya imani hayafai kulazimishwa.

Hivyo katika nchi kama Misri Wakristo waliotafuta uhuru wa kisiasa walilazimishwa kuwa chini ya Askofu wa Bizanti, wakajisikia wanagandamizwa kidini pia, si kisiasa tu. Waarabu Waislamu walipofika walikaribishwa mahali pengine kama wakombozi wanaomaliza utawala wa kidikteta. Waliwaahidi vikundi vyote vya Wakristo uhuru wa dini. Ahadi hiyo ilitimizwa kwa namna tofauti.

Utawala wa Kiislamu ulifikia nchi hizo kwa njia ya vita. Mwanzoni walikuwa Waarabu kadhaa tu: walichukua madaraka ya serikali kuu na kujenga makambi ya kijeshi katika kila nchi. Vijana wa Kiarabu walifuata baba zao wakiitikia wito wa dini uliokuja pamoja na nafasi ya kupata maisha nafuu. Walifundishwa kwamba ikiwa watakufa vitani watapokewa na Mungu kama mashahidi wa imani na kuingia Paradiso moja kwa moja. Lakini wasipokufa vitani watakuwa matajiri wakitawala nchi mpya na kupokea kodi za wenyeji wasio Waislamu. Imani ya aina hii iliwapa nguvu kweli na iliendelea kuvuta Waarabu wengi kutoka kwao kuhamia Afrika Kaskazini na Asia ya Kati.

Chini ya utawala wa Waarabu Waislamu, wenyeji waliruhusiwa kuendelea na desturi zao lakini hawakuwa na haki zote za uraia. Wasio Waislamu walijiona wanabaguliwa mbele ya Waislamu. Walitozwa kodi kubwa ya pekee. Mahakamani hawakuweza kushuhudia dhidi ya Mwislamu, walilazimishwa kuvaa nguo za pekee tofauti na Waislamu, walikataliwa kupanda farasi, kujenga makanisa mapya, au kutumia kengele makanisani.

Waislamu walipata kipaumbele katika mambo yote. Hivyo polepole wenyeji walianza kutumia lugha ya Kiarabu pamoja na kujiunga na Uislamu. Bila shaka wazazi wengine walitumaini kuwasaidia watoto wao wapate maendeleo maishani wakifuata dini ya watawala.

Masharti ya kujiunga na Uislamu yalikuwa rahisi sana. Hakuna mafundisho magumu, mwanzoni inatosha kutamka "shahada" ya Kiislamu ambayo ni fupi sana: As-haddu inna la ilaha ila allah, wa Muhamad rasul ullah. (Nakiri ya kwamba Mungu ndiye mmoja tu, na Mohamad ni mtume wa Mungu). Lakini baadaye haikuwezekana kurudi katika Ukristo maana sheria ya Kiislamu iliruhusu Mkristo kugeuka Mwislamu lakini ilikataza kwa adhabu ya kifo Mwislamu asitoke katika imani hiyo na kufuata dini nyingine.

Kwa kawaida Wakristo hawakulazimishwa kuacha imani yao. Viongozi wa Waarabu washindi walifanya mikataba na maaskofu wa Kikristo katika maeneo waliyoyateka. Wakristo waliahidiwa ulinzi wa makanisa yao wakiambiwa wanaweza kuendelea na mila na desturi walivyozoea.

Lakini mara kwa mara upande wa watawala na wakubwa yalijitokeza matendo mabaya, kama makanisa kubomolewa au kugeuzwa misikiti, n.k. Kwa mfano msikiti mkuu wa Dameski (Siria) ulikuwa zamani Kanisa la Mt. Yohane Mbatizaji. Mwanzoni Waarabu waliahidi kuliheshimu, lakini mtawala aliyefuata alitaka jengo kubwa lililopatikana mjini kwa ajili ya ibada yake. Ndivyo ilivyotokea Waturuki walipoteka Konstantinopoli. Kanisa Kuu la Hagia Sofia (Hekima Mtakatifu) liligeuka msikiti.

Vipindi vya kulazimisha vilitokea tena na tena, hasa baada ya mataifa mapya kuwa Waislamu. Waarabu wenyewe walionyesha ustahimilivu zaidi kwa wenye imani nyingine (Wakristo, Wayahudi, Wafuasi wa dini ya Uajemi n.k.). Lakini Waturuki, Waajemi na Wamongolia baada ya kuwa Waislamu walikuwa wakali.

Hasa vipindi vya vita kati ya Wakristo kutoka Ulaya na Waarabu viliongeza uchungu kwa Wakristo chini ya utawala wa Kiarabu. Katika vipindi hivyo Wakristo chini ya Waislamu waliweza kuangaliwa kama wasaliti na kuteswa, makanisa yao kubomolewa, n.k.

Kwa ujumla majaribio ya vita vya msalaba ya kuikomboa nchi takatifu yalishindikana. Pamoja na hayo vita hivyo vilidhoofisha Wakristo wa Mashariki waliozoea kuishi chini ya Waarabu Waislamu. Ilibidi walipe madeni yaliyoachwa nyuma na ndugu zao kutoka Ulaya Magharibi.

Katika uhusiano mgumu kati ya dini hizo mbili kule Ulaya na Mashariki ya Kati, Waislamu wanastahili pia sifa. Ahadi nyingi walizozifanya zilivunjika, lakini mahali pengine Wakristo walipewa nafasi za kuendelea kuishi kati ya Waislamu hata kama ilikuwa kwa ubaguzi na mateso.

Maisha yao yalikuwa mara nyingi magumu, lakini mahali pengi waliweza kubaki. Waliruhusiwa kuendelea na ibada zao (lakini waliweza kukataliwa kujenga makanisa au hata kutengeneza makanisa ya kale isipokuwa kwa kulipa tena kodi za nyongeza). Katika mambo ya ndoa au urithi wa mali walikuwa chini ya makanisa yao.

Viongozi wa makanisa yao waliwajibika mbele ya serikali ya Kiislamu juu ya ushirikiano mwema. Kwa namna hiyo jumuiya za makanisa kama vile la Kigiriki, la Kikopti, la Kisiria, la Kiarmenia n.k. zilihifadhiwa mpaka leo katika nchi za Kiarabu, isipokuwa idadi ya waumini wao iliendelea kupungua. Tena Wakristo walianza kuhamia nchi ambako watakuwa raia huru bila kasoro.

(..........)

Maoni blog yetu : Kutokana na hatua hii ya maandishi haikutajwa tena katika Kanisa la Orthodox. Unaweza kusoma zifuatazo :

Kanisa la Orthodox na Kanisa Katoliki
Umonaki katika Kanisa la Orthodox 
KUTAFUTA IMANI LAKUNYOLOKA – AMA KI ORTHODOKSI
Wamisionari tano halisi ambaye heri Afrika kusini mwa Sahara (na takatifu mtoto bila majina ya Afrika)

 

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου